Maaskofu wa IMBISA kuanza kutumia mitandao ya kijamii kutuma ujumbe wa haki, amani
na upendo!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, hivi karibuni
limehitimisha semina maalum iliyojikita katika matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii
inayoendelea kushika kasi kwa umaarufu, wepesi na kasi ya kuweza kuwafikia watu wengi
kwa mkupuo, ikilinganishwa na njia za mawasiliano zilizozoeleka kama sehemu ya mapokeo.
Maaskofu katoliki kutoka Zimbabwe, baada ya kujifunza na hatimaye kuanza kubobea
katika matumizi ya mitandao ya kijamii, wameamua kwamba, wakati wa mchakato wa uchaguzi
mkuu nchini Zimbabwe watajitahidi kutumia kikamilifu mitandao hii ili kusambaza ujumbe
wa amani, upendo, upatanisho na mshikamano wa kitaifa. Kwa njia ya mitandao, Maaskofu
wataweza kuwafikia wananchi wa Zimbabwe wakiwa katika maisha yao ya kawaida, kuliko
ilivyokuwa hapo hawali walipokuwa wanawasubiri wanapokwenda Kanisa siku za Jumapili.
Huu
ni ufafanuzi kadiri ya taarifa za Shirika la Habari za Kanisa Barani Afrika, CISA,
ambao umetolewa na Padre Richard Menatsi, Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano IMBISA.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini Mwa Afrika, IMBISA linaonya kwamba,
uchaguzi wa kidemokrasi haupaswi kamwe kuwa ni chanzo cha kinzani, vurugu na vita;
lakini haya nimambo ambayo yamekuwa yakijitokeza sehemu mbali mbali Barani Afrika;
daima waathirika ni raia na wanyonge ndani ya Jamii.
Umwefika wakati kwa wananchi
Barani Afrika kujifunza kutumia kura zao kama njia makini inayoonesha utashi wa kisiasa
unaopania kuleta mabadiliko. Ni wakati wa kujenga na kuimarisha misingi ya haki na
amani na kwamba, matumizi ya mtutu wa bunduki ni mwelekeo ambao umepitwa na wakati!