Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya sita ya Kipindi cha Pasaka
Tunaendelea na Tafakari ya Neno la Mungu, tayari tukiwa Dominika ya VI katika siku
za furaha na nderemo, Mama Kanisa atuwekea Neno la furaha, Neno ambalo latufundisha
kuwa Roho Mtakatifu ndiye mwalimu wa ukweli wote!
Katika somo
la kwanza tunapata kuona Jumuiya ya kwanza ambayo ni mchanganyiko wa Wakristo waliotokea
dini ya kiyahudi ambao wanasisitiza tohara na Wakristu waliokuwa wapagani ambao jambo
hili kwao si la msingi. Kumbe kutokana na makundi haya mawili kuwa na mlengo tofauti
kunakuwepo na matatizo ya hapa na pale.
Shida kubwa ambayo inashika kasi ni
ile ambayo wapagani wanalazimishwa kuwa kwanza Wayahudi yaani kutahiriwa kwanza na
ndipo waingie ukristu. Wapagani wanakataa hilo wakisema wokovu unatoka kwa Kristo
na si toka mila za Kiyahudi. Mt Paulo anaona ni vema na sahihi kila mmoja kumfuasa
Bwana akitokea kwenye utamaduni wake bila kulazimishwa kupitia utamaduni wa mwingine.
Mt. Petro na Yakobo bado wanayo alama ya kiyahudi na hivi wamelala katika upande wa
kutahilriwa kwanza kabla ya kuwa mkristo.
Mpendwa msikilizaji, shida hii itatatuliwa
pamoja na shida nyingine kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, yaani wataitisha Mtaguso
wa Kwanza wa Yerusalemu. Basi, wanaamua kwa pamoja kuwa watafundisha Injili ya Bwana
katika tamaduni zao, na kusisitiza kuwa mkristo hata hivyo ana haki ya kukataa mila
fulani katika utamaduni wake, yaani kama kinapingana na Injili ya Bwana.
Kumbe,
baada ya Mtaguso basi wokovu upo pasipo kutahiriwa cha msingi kumfuasa Kristo katika
mapendo ya kweli. Kushika vema taratibu za ndoa takatifu, taratibu za kumtolea Mungu
sadaka ambazo zinaambatana na mapendo kwa jirani na Mungu mwenyewe.
Katika
somo la pili tunapata kuona faraja ambayo wataipata wale wote watakaoteseka kwa ajli
ya Neno la Mungu na imani kwa ujumla. Mwishoni mwa nyakati uzima wa kimungu utakuwa
ndani yao wote ambao wametoa jasholao kwa kumpenda Mungu. Mt Yohane yuko katika ndoto
anaona mji wenye pande nne na milango3 kila upande, vikiwa ni alama ya uwezekano wa
wokovu kwa wote (maana ya namba 4 katika Biblia-Nzima, wote) na milango yaashilia
uwezekano wa kuingia katika uzima wa milele. Huko mbinguni hakutakuwa na litrujia
wala mahekalu bali kumwona Mungu uso kwa uso. Tazama mpendwa furaha gani hiyo kuweza
kumwona Mungu!
Ili tuweze kufikia mapendo na furaha ya mbinguni kadiri ya kitabu
cha Ufunuo lazima tutekeleze yale ambayo Mwinjili anatuambia. Anasema mtu akinipenda
mimi, akilishika Neno langu, mimi na Baba yangu tutakuja kwake. Kumbe, yatupasa kujenga
umoja na Baba mapema hapa duniani. Na hakuna njia nyingine ya kwenda kwa Baba pasipo
Kristo anayesma anionaye mimi amwona Baba. Yatupasa kuamini kina kazi za Kristo na
mausia yake kwa ajili ya kufika kwa Baba. Neno la Mungu ni Kristo mwenyewew anayesema
nasi kila siku kumbe tulipende tuliishi.
Mpendwa ona jinsi Kristo anavyotupenda
kabla hajaondoka anahaidi Roho Mtakatifu ambaye atatufundisha yote, atakuwa mwalimu
mfariji wetu. Hapa twaweza kuweka swali hivi Yesu hakufundisha yote? Alifundisha yote
lakini mazingira yanabadilika na hivi tunahitaji msimamizi wa siku zote atakayeongoza
historia mpaka mwisho wa nyakati. Mt. 28. Kristo anahaidi amani , si kama ile itolewayo
na dunia kwa njia ya mabavu bali ijayo kama tunda la Pasaka, tunda la Roho mfariji,
Roho wa amani.
Mpendwa, nikutakie furaha tele ya Pasaka ukijiandaa kwa ajili
ya Sherehe ya kupaa Bwana Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa
kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.