Sala ya Papa Francisko kwenye kaburi la Mtakatifu Francisko wa Assisi
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 2 Mei 2013 amesali kwenye kaburi la Mtakatifu
Francisko wa Assisi kwa njia ya "webcam" na kumwomba Mtakatifu Francisko aweze kuiombea
mioyo ya waamini ili iwe na amani.
Anawaomba Wafranciskani kusali kwa ajili
ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kuwasaidia waamini
na watu wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa na Ulimwengu
katika ujumla wake.
Baba Mtakatifu ameoneshwa pia toleo maalum la jarida linalochapishwa
na Wafranciskani ambalo limetolewa kuonesha yale yaliyojiri wakati wa kuchaguliwa
na hatimaye kuanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu ameonesha
utashi wa kutembelea mji wa Assisi, makao makuu ya Wafranciskani, mahali ambapo watu
wengi wanakwenda kufanya hija ya imani, lakini zaidi kwa ajili ya kuombea amani kati
ya watu na amani katika mioyo ya binadamu.
Akizungumzia kuhusu tukio hili la
Baba Mtakatifu Francisko kusali moja kwa moja kwenye kaburi la Mtakatifu Francisko
wa Assisi, Padre Enzo Fortunato anasema, hii inaonesha umuhimu wa njia mpya za mawasiliano
ya kijamii zinavyoweza kutumika kama vyombo vya kusaidia kukuza na kuimarisha imani,
lakini zaidi kama vyombo vya Uinjilishaji mpya, kama inavyojionesha kwa idadi kubwa
ya sala zinazotumwa kwenye kaburi la Mtakatifu Francisko wa Assisi kutoka pande mbali
mbali za dunia.
Tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe, watu wengi wamejielekeza
zaidi katika sala ya matumaini na mshikamano katika hija ya imani wakati huu Mama
Kanisa anapoadhimisha mwaka wa Imani.