2013-05-03 07:45:31

Mtumishi wa Mungu Franciska Paula de Jesus kutangazwa kuwa Mwenyeheri huko Brazil


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko; Jumamosi, tarehe 4 Mei 2013, anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Franciska de Paula de Jesus aliyeishi kunako mwaka 1810 hadi mwaka 1895 kuwa Mwenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu itakayofanyika mjini Baependi, Brazil. RealAudioMP3

Ni mwenyeheri anayefahamika sana nchini Brazil na kwamba, hii ni zawadi kubwa ambayo Baba Mtakatifu Francisko analipatia Kanisa nchini Brazil linapojiandaa pia kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Kardinali Amato anasema kwamba, Baba Mtakatifu anawafahamu fika wananchi wa Brazil; imani na upendo wao kwa Yesu anayewakirimia furaha ya kweli katika maisha sanjari na Ibada kwa Bikira Maria, bila kusahau upendo wanaouonesha kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ni waamini wenye moyo wa ukarimu, wako tayari kupokea Injili ya Uhai inapotangazwa kwao; hawa ni watu wenye heshima, upendo na mshikamano wa kidugu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Wanathamini usawa kati ya watu na kwamba, wako makini katika kulinda na kutunza mazingira. Huu ndio utajiri unaofumbatwa katika maisha ya kiutu na kiroho, kiasi kwamba, wananchi wa Brazil wanajikisia kwa namna ya pekee kwamba, wamebarikiwa.

Hizi ni tunu ambazo Mwenyeheri Franciska Paula de Jesus aliziishi na kuzimwilisha katika hija ya maisha yake hapa duniani; akawaachia kama urithi wananchi wa Brazil na kwa ajili ya Kanisa zima.

Mwenyeheri Franciska alizaliwa kwenye Familia ya Watu waliokuwa utumwani Brazil, lakini baadhi ya ndugu zake wakabahatika kupata utajiri wa mali ambayo aliachiwa urithi ambao aliutumia kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Baadhi ya fedha hizi zilitumika kujengea Kikanisa cha Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Akajiweka wakfu kama bikira na kuyatoa maisha yake kwa ajili ya huduma ya upendo na sala kama alivyokuwa ameshauriwa na Mama yake mzazi kabla ya kuaga dunia.

Hakujiunga na Shirika lolote la kitawa, akabaki mwaminifu katika nadhiri zake kama ilivyokuwa hata kwa wanawake wengine wa nyakati zake, waliotolea maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakiwa nyumbani kwao, waliendelea kuwasaidia maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Akafariki dunia tarehe 14 Juni 1895 katika hali ya utakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Franciska de Paula de Jesus kuwa Mwenyeheri anasema kwamba, kwa hakika alikuwa ni mwamini mlei aliyejitoa bila ya kujibakiza katika maisha ya sala, akadhihirisha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini wa kiroho na kimwili.

Ni mwanamke aliyekuwa na Ibada kwa Bikira Maria, kiasi kwamba, Rozari ilikuwa daima mikononi mwake. Alitumia muda wake mwingi kwa ajili ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na kufanya tafakari juu ya Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo. Bikira Maria kwake alikuwa ni Mama mfariji, kiasi kwamba, ile sala ya Salam Malkia “Salve Regina” ikawa ni sala na wimbo wake wa daima.

Watu wengi walimwendea kumshukuru kutokana na neema na baraka walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya maombezi yake, lakini daima aliwaambia kwamba, anasali na kuwaombea kwa Bikira Maria anayemsikiliza.

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu anahitimisha maoni yake kuhusu mwenyeheri Franciska kuwa ni mwamini mlei aliyebahatika kuishi katika utakatifu wa maisha na kwa hakika tukio la kumtangaza kuwa Mwenyeheri linadhihrisha ushuhuda wa maisha halisi ya Kikristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.