Karibu tena Papa mstaafu Benedikto XVI mjini Vatican!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Alhamisi, tarehe 2 Mei 2013 amerejea tena mjini
Vatican baada ya kuishi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo kwa takribani miezi
miwili na kuelekea kwenye makazi yake mapya yaliyoko kwenye Monasteri ya Mater Ecclesiae
mjini Vatican.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipowasili
kwenye uwanja wa ndege mjini Vatican amepokelewa na viongozi waandamizi kutoka Vatican
wakiongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali.
Msafara wa viongozi
hawa ulipowasili kwenye lango la Monasteri ya Mater Ecclesiae umepokelewa na Papa
Francisko kwa upendo, mshikamano na udugu. Viongozi hawa wawili walielekea kusali
kwa pamoja kwenye Kikanisa kilichoko ndani ya Monasteri hii ambayo kwa sasa yatakuwa
ni makazi ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika hija yake maisha hapa duniani, akitumia
muda wake mwingi kwa ajili ya kusali, kutafakari na kujisomea. Baba Mtakatifu mstaafu
alisema mwenyewe kwamba, kwa sasa anapenda kuutumia muda wake kwa ajili ya kusali
ili kuliombea Kanisa.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto katika makazi haya
mapya ataendelea kuishi na Askofu mkuu Georg Gaenswein na Watawa waliokuwa wanatoa
huduma wakati alipokuwa kwenye Makazi ya Kipapa mjini Vatican katika kipindi cha uongozi
wake.