Kanisa ni Jumuiya ya waamini inayopaswa kusimikwa katika upendo, mshikamano na udugu!
Kanisa halina budi kusikiliza kwa makini maongozi ya Roho Mtakatifu na kujitahidi
kuyamwilisha katika maisha na utume wake kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, huku
wakitambua kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya
dunia, lakini, linapaswa kuwa imara na thabiti ili lisimezwe na malimwengu.
Ni
Roho Mtakatifu ambaye amewawezesha Wakristo wa Kanisa la mwanzo kujifunga kibwebwe
na kuanza kutoka katika miji yao, kifua mbele ili kumtangaza Yesu aliyeteswa, akafa
na kufufuka kutoka katika wafu. Roho Mtakatifu anahamasisha, anajenga na kuliimarisha
Kanisa kutoka katika undani wake, huu ni mchakato endelevu unaojionesha hata leo hii
katika maisha na utume wa Kanisa.
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na
Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 2 Mei 2013 katika Ibada ya Misa Takatifu
aliyoiadhimisha kwenye Kikanisa cha Domus Sancta Marthae kilichoko mjini Vatican na
kuhudhuriwa na wafanyakazi kutoka katika Gazeti la L'Osservatore Romano linalomilikiwa
na Vatican. Waamini wa Kanisa la mwanzo anasema Baba Mtakatifu walikabiliana matatizo
na changamoto mbali mbali kutokana na kizani za mawazo na baadhi ya waamini kudhani
kwamba, walikuwa wanaupendeleo wa pekee kabisa machoni pa mwezi Mungu kiasi hata cha
kutaka kuwadharau na kuwabeza jirani zao.
Roho Mtakatifu akatekeleza wajibu
wake: umoja, upendo, udugu na mshikamano ukapatikana miongoni mwa waamini kiasi cha
kujiachilia kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo, wakiwa wepesi kuchanja mbuga
ili kuwashirikisha wale wasiomwamini Kristo ile furaha ya kuwa kweli mfuasi wa Kristo
si tu kwa maneno bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha.
Wakristo wanachangamotishwa
na Kristo mwenyewe kujishikamanisha katika kifungo cha upendo ambacho ni kielelezo
makini na utambulisho wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Jambo hili linawezekana ikiwa kama
Wakristo watamwilisha ndani mwao na katika vipaumbele vyao Amri za Mungu ambazo kimsingi
ni dira na mwongozo wa maisha adili. Waamini wajifunze kuishi katika upendo, daima
wakitafuta toba na wongofu wa ndani, ili kuendelea kufaidi neema inayobubujika kutoka
kwa Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Waamini wajifunze pia kusamehe na kusahau;
huku wakimwilisha huruma na upendo huu kwa njia ya matendo ya huruma hasa kwa wale
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Hii inatokana na
ukweli kwamba, waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani wanakabiliana na dhambi
pamoja na vishawishi kadha wa kadha.
Waamini watambue ubinadamu wao na wawe
wepesi kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Kanisa
liendelee kufungua malango ya matumaini kwa wote wanaotaka kuonja upendo wa Mungu!