2013-05-03 11:49:31

Kanisa linawahitaji Wakristo wenye ujasiri wa kutangaza na kuishuhudia Injili ya Kristo bila woga!


Wakristo wanaalikwa kuwa na ujasiri wa kutangaza na kuishuhudia imani yao bila woga katika medani mbali mbali za maisha; wakitambua kwamba, wanapaswa kudumu katika sala na imani; hata pale wanapokabiliana na madhulumu kama yalivyowakuta Mitume wa Yesu katika maisha yao.

Imani ambayo Wakristo wameipokea walipobatizwa, wanapaswa kuiungama, kuiadhimisha, kuirithisha na kuishuhudia katika hija ya maisha hapa duniani. Kwa njia ya imani katika Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, waamini wamekirimiwa zawadi ya kusamehewa na kuondolewa dhambi zao kiasi hata cha kupatanishwa na Mwenyezi Mungu. Imani hii inapaswa kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Ijumaa, tarehe 3 Mei 2013 kwenye Kikanisa cha Domus sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican, kama sehemu ya mwendelezo wa Baba Mtakatifu kufahamiana kwa karibu zaidi na wafanyakazi wa Vatican.

Watoto wafundishwe na kurithishwa amana za imani ya Kanisa kwamba, Kristo ni hai kati ya wafuasi wake na kwamba, hiki ndicho kiini cha Habari Njema. Wasichoke kumwendea Yesu kwa njia ya sala pamoja na kushiriki mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Waamini wajijengee utamaduni wa kusali na kudumu katika sala ili kuzungumzana na Kristo. Ili kufanikisha azma hii kuna haja ya kuondokana na ubinafsi na wivu ambao hauna tija wala maendeleo kwa Kanisa la Kristo.

Ibada hii ya Misa Takatifu katika kumbu kumbu ya Mitume Filipo na Yakobo. imehudhuriwa na wanajeshi wa vikosi kwa ulinzi na usalama "Swiss Guards". Mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, Papa Francisko amewashukuru: kwa uaminifu, kazi, upendo na ushuhuda wao wa Kikristo kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanis kwa ujumla.







All the contents on this site are copyrighted ©.