2013-05-02 09:31:02

Waamini wanamsubiri Papa Francisko kusali Rozari pamoja naye, Jumamosi tarehe 4 Mei 2013


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Mei 2013, Saa 12:00 jioni, anatarajiwa kusali Rozari takatifu na waamini watakaokuwa wamekusanyika katika Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Itakumbukwa kwamba, hii ni mara ya pili kwa Baba Mtakatifu Francisko kwenda Kanisa hapo tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Lakini wakati huu, anakwenda rasmi kama sehemu ya utekelezaji wa mzunguko wa hija kwa Makanisa makuu yaliyoko mjini Roma. Mara atakapofika Kanisani hapo atapewa Msalaba na kuubusu baadaye atakwenda kutoa heshima kwa Sanamu ya Bikira Maria Afya watu wa Roma "Salus Popoli Romani" kama inavyojulikana kwenye viunga vya Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu.

Ibada ya Rozari Takatifu ambayo kimsingi ni muhtasari wa Injili itaendeshwa kwa lugha ya Kiitalia, wakiongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Jumamosi ijayo, Kanisa litatafakari Matendo ya Utukufu.

Akihojiwa na Gazeti la L'Oservatore Romano linalotolewa na Vatican kila siku, Padre Fernàndes Rodriguez, mkuu wa Mapadre wauungamishaji wanaotoa huduma yao kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu mjini Roma anasema kwamba, kwa sasa wako Wadominikani kumi na wawili wanaotekeleza wajibu na utume wao chini ya uongozi wa Baraza la Toba ya Kitume.

Ni utume unaohitaji hekima ya maisha ya kiroho, kwa kuwaheshimu na kuwajali wale wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho ili kuwasaidia kuonja upendo huu kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Jumuiya hii ya Mapadre Wadomenikani bado wanayo kumbu kumbu hai asubuhi na mapema, tarehe 14 Machi 2013 Papa Francisko alipofika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu kutolea heshima yake kwa Mama wa Mungu na Kanisa, akaacha shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria.

Uwepo wake tena ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali na kumwombea katika maisha na utume wake; ili aweze kuwa na afya ya roho na mwili pamoja na kuendelea kuwaimaarisha ndugu zake katika imani, matumaini, mapendo na umoja kamili.

Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea kwa mara ya kwanza katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, aliwataka waungamishaji kuwa na huruma na mapendo. Padre ambaye anatumia muda wake mwingi kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, inakuwa kweli ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia watu wake. Sakramenti ya Upatanisho inawahitaji Mapadre watakatifu, wanaotambua dhamana na wito ambao wamekabidhiwa na Mama Kanisa.

Utume huu unapaswa kutekelezwa katika hali ya sala na ukimya. Mapadre pia watambua umuhimu wa kujipatanisha na Mungu kabla ya kuwapatanisha wengine, ili pia waweze kuonja huruma na upendo unobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho.







All the contents on this site are copyrighted ©.