2013-05-02 14:33:23

Siku kuu ya Vesakh: pendeni, lindeni na kudumisha uhai wa binadamu


Wakristo na Wabudha wanahamasishwa kupenda, kulinda na kudumisha uhai wa binadamu, ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe kutoka kwa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa waamini wa dini ya Kibudha wanaposherehekea Siku kuu ya Vesakh kwa mwaka 2013. Huu ni mwendelezo wa mchakato unaopania kwa namna ya pekee kudumisha uhusiano wa kidini na kirafiki na waamini wa dini ya Kibudha.

Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, alikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, kwa kutambua kwamba, Kanisa lina dhamana kwa ulimwengu katika harakati za kupenda, kulinda na kuendeleza kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu.

Lengo ni kuwasaidia: maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; wanaoteseka na kudhulumiwa ili waweze kupata haki, amani pamoja na kudumisha upatanisho.

Ili amani iweze kupatikana na kushamiri miongoni mwa watu wa mataifa kuna haja kwanza kabisa kuheshimu, kuthamini na kulinda zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake. Hivi ndivyo alivyokuwa ameandika Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake wa kuombea amani duniani kwa mwaka 2013.

Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika ujumbe huu anabainisha kwamba, Kanisa Katoliki linaheshimu na kuthamini Mapokeo ya Dini ya Kibudha hasa katika kuheshimu uhai wa binadamu, taamuli, ukimya na ukawaida unaojionesha katika uhalisia wa maisha. Majadiliano ya pamoja baina ya waamini wa dini hizi mbili yanaonesha kwa namna ya pekee jinsi ambavyo wanaheshimu zawadi ya uhai.

Hii ni changamoto ya kuondokana na utamaduni wa kifo, kwa kukazia: maadili, utu wema, upendo kwa jirani pamoja na Amri za Mungu. Kanisa Katoliki linathamini na kuenzi yale ambayo ni kweli na matakatifu yanayopatikana kwenye dini nyingine. Kutokana na changamoto iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa, Wakristo na Wabudha wakishirikishana amana za Mapokeo yao ya kidini wanapaswa kujenga na kudumisha mazingira ya kupenda amani, kulinda na kutetea uhai wa mwanadamu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ya binadamu ni jambo takatifu, lakini limeendelea kukabiliana na kinzani kutoka kwa watu binafsi na Jamii za watu, changamoto kwa waamini wa dini hizi mbili kusimama kidete kupinga mambo yote yanayohatarisha uhai wa binadamu, kwa kuamsha tena dhamiri na maadili mema ndani ya Jamii ili watu kweli waweze kupenda, kulinda na kuenzi uhai wa mwanadamu katika hatua zake zote.

Kardinali Jean Louis Tauran anahitimisha ujumbe katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Vesakh kwa kuwataka Wabudha kuendelea kushirikiana kwa kuguswa na mahangaiko ya Familia ya binadamu kwa kuenzi utakatifu wa maisha ya mwanadamu. Na kwa maneno haya, anawatakia waamini hao amani na furaha wanapoadhimisha Siku kuu ya Vesakh.







All the contents on this site are copyrighted ©.