Sakramenti ya Ubatizo ni mlango wa Imani kwa Kristo na Kanisa lake!
Nyumba inaweza kuwa nzuri utakavyo lakini bila mlango ni bure. Gari na vyombo vyote
vya usafiri vinaweza kuwa vya muhimu sana lakini bila milango havifai kitu. Mlango
ni chombo kinachokuingiza katika mahusiano na vitu vingine. Ndani ya pipa
letu vijana leo hewani tunachomoka na maana ya Porta Fidei, Mlango wa Imani. Seat
bado zipo, karibu ndani, chukua nafasi, funga mkanda vizuri tuanze kupaa ndani ya
studio za Radio Vatican. Ubatizo ni Sakramenti, ishara wazi ya neema isiyoonekana.
Ubatizo unatuondolea dhambi ya asali pamoja na adhabu zake, unatufanya kuwa watoto
wa Mungu na Kanisa. Kumbe kijana unatakaswa kwa Sakramenti hii, na unaingia katika
mahusiano kati yako na Kanisa na kati yako na Mungu. Mlango huu ukishaupita hakuna
kurudi nyuma. Hata ukianza kutapatapa mara uende huku mara kule mara ukashifu dini
na kadhalika, wewe unabaki mkristo, sababu umebatizwa. Ukiwa ndani ya mahusiano na
Mungu unapaswa kujitahidi kutunza vema mahusiano hayo. Fungua moyo na akili yako
ili kumpokea Kristo na kudumu naye. Safari yako ya mahusiano, safari ya muungano kati
ya Mungu inaanza na Ubatizo na inadumu milele iwapo utaishi kwa uaminifu siku zote.
Mahusiano hayo unayoanza hapa duniani yanaendelea katika uzima wa milele. Bila
shaka unajiuliza, unahitaji nini katika mlango huu na muunganiko wako na Mungu. Katika
Kanisa la Mungu unapobatizwa, unabatizwa kwa kuzingatia Imani uliyo nayo kwa Mungu.
Bila Imani ubatizo huo hauna nguvu, sababu ubatizo ni mlango unaokuingiza katika safari
ya Imani na mahusiano ya kudumu na Mungu. Kumbe unaalikwa kuikiri imani sio tu unapobatizwa,
bali kila siku ya maisha yako. Imani hiyo uikiri kwa moyo radhi. Imani hiyo haiishii
kuikiri kanisani tu, au kwa maneno tu. Imani hiyo uikiri kila wakati na kila mahali
unapojikuta. Uwe kazini, shuleni, sokoni, sehemu ya biashara, nyumbani, safarini na
kadhalika. Ikiri Imani yako kwa matendo pia. Mtume Yakobo anatufundisha: yafaa nini
imani yako iwapo unaikiri kwa maneno tu lakini hauishuhudii kwa matendo. Kumbe matendo
yako ni ya msingi sana. Onesha wazi kwa matendo ya kuwa wewe ni mkristu unaishi maadili
ya kikristu bila aibu bila woga. Tena jisikie fahari juu ya imani yako, ukiweza kuzingatia
hilo utakuwa mtu wa furaha sana. Baada ya kuingia katika muungano na Mungu kwa
Sakramenti ya Ubatizo, unadumu katika mahusiano hayo kwa Sakramenti zingine. Kila
Sakramenti ni ishara wazi ya neema ya Mungu isiyoonekana. Huwezi kupokea kwa halali
Sakramenti yeyote bila kuwa umebatizwa. Mwenyezi Mungu amejishusha na kuamua kuwa
na mahusiano na muungano nawe kwa njia mbali mbali na katika nyakati tofauti. Hii
yote ni sababu anakupenda. Kumpokea kwako katika Sakramenti ya Ubatizo, mlango wa
imani. Kudumu kwako ndani yake kunaongozwa na Upendo. Upendo ulio nao kwake Mungu
ni upendo huo huo uwe nao kwa wengine bila ubaguzi. Ukisema unampenda Mungu bila
kuwapenda wengine utakuwa muongo. Na ukisema unatenda mema kwa wengine bila kuishi
maadili ya kikristu na kumwamini Mungu pia utakuwa muongo. Mkiri na kumwamini Mungu
kwa upendo wa kweli, kwa moyo radhi na akili timamu. Mlango wa moyo wangu umefunguliwa
na Kristu ili kumpenda Mungu na kuwapenda watu wote. Nakualika wewe pia ufungue mlango
wa moyo wako na udumu katika hilo. Ndivyo ninanvyosepa kutoka Studio za Radio Vatican,
sauti ya kinabii Padre Celestine Nyanda.