Ushuhuda wa imani katika Familia, sehemu za kazi na kwenye Jumuiya!
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, inaendelea
kukushirikisha Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha Kwaresima
kwa Mwaka 2013. Leo tunagusia kuhusu ushuhuda wa imani katika: familia, sehemu za
kazi na katika Jumuiya. Kutujuza zaidi ndani ya viunga vya Radio Vatican ni Sr. Gisela
Upendo Msuya. Imani ya kweli
inapimwa kupitia “afya” ya familia na ya jamii. Haya mawili yanategemeana. Imani isipojidhihirisha
katika uhai wa familia, iliyo Kanisa la kwanza, la nyumbani na la msingi, itakuwa
ni vigumu kujidhihirisha popote. Familia zetu zinazidi kuwa legelege kwa sababu hazichukuliwi
tena kuwa eneo la malezi muhimu ya kiimani na ya kiutu. Malezi ya familia “yamebinafsishwa”
katika tendo la kuamini kila mtu katika familia ana wajibu wa kujilea mwenyewe bila
ya msaada wa mwingine kati ya wale wanaounda familia moja. Katika mazingira ya
namna hii, dhana nzima ya familia inapotea na familia inapoteza fursa ya kuwa “shule
ya imani”, ambamo wazazi na watoto, kwa pamoja, wanakua katika imani. Mwaliko huu
wa Mtume Paulo kwa Kanisa la Korintho ni mwaliko kwanza kwa hili “Kanisa la nyumbani”.
Tunazihimiza familia zote za Kikristo kuizingatia imani kwa dhati: Familia, “Simameni
imara katika imani”! Ipelekeni nyumbani ile imani mliyoipokea kutoka kwa Mungu kupitia
Kanisa lake. Humo mkaiishi na kuijengea mazingira ya kukua. Hili linapotekelezwa,
familia itakuwa na uwezo wa kuipeleka imani katika jamii. “Familia inapata katika
mpango wa Mungu Mwumbaji na Mkombozi sio tu utambulisho wake; yaani, yenyewe ni nini,
bali pia utume wake; yaani, ni nini inachoweza na inachopaswa kufanya”. Familia zinapoutambua
utambulisho wake na utume wake zinaweza kuiishi imani kwa namna bora zaidi. Huo unakua
ndiyo mwanzo wa ushuhuda wa kikristo. Ndani ya familia panakuwa ni mahali unamozaliwa
moyo wa huruma kwa wanyonge na wasiojiweza. Humo imani inakuwa ni jibu la kutatua
hali za kutoelewana katika familia. Ni kwa namna hii tunaweza kupiga hatua ya
kwanza katika kuboresha mazingira ya mahali tunamoishi, kwa sababu “familia ni mahali
panapofaa pa kujifunzia na kuzoeshwa utamaduni wa msamaha, amani na upatanisho”. Kwa
sababu hiyo wajibu wa malezi endelevu ya imani katika familia unapaswa kuwa wa kudumu.
Kwa namna hii tunaweza kuanza kupiga hatua ya kwanza katika kupambana na maradhi hatari
kama UKIMWI, kupambana na rushwa, uzembe, na tabia zote ambazo zina athari mbaya kwa
makuzi ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Kwa njia ya imani familia zitapata furaha
ya kweli inayojengwa kupitia fadhila za amani na upendo. Kazini na katika Jumuiya Mwaliko
wa kusimama imara katika imani hauishii kanisani na katika familia tu, ila unaanzia
hapo na kutoka hapo mwaliko huu unatekelezwa popote tunapokwenda. “Kukiri kwa mdomo
inaonesha kuwa imani inamaanisha ushuhuda na wajibu wa hadharani pia. Mkristo hatakiwi
kamwe kufikiri kuwa imani ni tendo la faragha. Imani ni kuchagua kusimama na Bwana
ili kuishi naye.” Kuipeleka imani katika jamii ni tendo la ushuhuda wa kikristo. Mtume
Yohane anatufundisha kuwa ni kwa njia ya imani tu ndipo tunaweza kuushinda ulimwengu:
“Na huku ndiko kuushinda ulimwengu: hiyo imani yetu” (1Yoh 5:4). Tendo la ushuhuda
wa mkristo linalojidhihirisha kwa njia ya imani halina maana ya kujaribu kuwalazimisha
watu wengine kuwa wakristo, bali ni kutia katika matendo misingi ya upendo, haki,
amani na maelewano kama Kristo anavyotuagiza, na kwa namna hii tunatakatifuza maeneo
ya kazi zetu za kila siku na jumuiya zetu. Huku ndiko kuwa chumvi na nuru ya ulimwengu.
Na Baba Mtakatifu Benedikto XVI anatuhimiza akisema: “Hatuwezi kukubali chumvi ipoteze
ladha au mwanga ubaki umefichwa (rej. Mt 5:13-16).” Imani ya kweli, ambayo inajidhihirisha
katika tendo la waamini kujitoa kama vyombo safi ambavyo Mungu anavitumia kuiumba
upya na kuitakatifuza dunia, ni chachu ya kweli kwa mwanadamu na kwa ulimwengu. “Je,
si kazi ya Kanisa kutoa mwanga wa Kristo katika kila kipindi cha historia? Si kazi
yake kufanya uso wa Kristo ung’are pia mbele ya vizazi vya hii milenia mpya?” Basi,
wakati huu wa Kwaresima ni wakati wa kuifanya upya imani yetu kwa njia ya Sakramenti
za Kanisa, hasa Sakramenti ya Upatanisho. Vile vile, huu ni wakati wa kufufua matendo
ya huruma na upendo na kuyafanya kuwa endelevu katika maisha yetu. Kanisa hapa
nchini linatambua “mchango mkubwa ambao wanawake na wanaume walitoa na kusaidia kukua
na kuendelea kwa jumuiya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.” Baba Mtakatifu Mwenyeheri
Yohane Paulo II atabaki kwetu kuwa ni tunda la utakatifu uliojidhirisha katika uaminifu
wake kwa Kristo aliyemtanganza na kumtumikia. Maisha yake ya sala, uvumilivu, uongozi
wake shupavu na msimamo wake usiotetereka katika kuitafuta na kuikazia macho sura
ya Yesu, imemfanya kuwa shahidi wa imani anayepaswa kuwa mfano wa kuigwa. Wapo
pia Watanzania wenzetu ambao maisha yao yalikuwa ni kielelezo cha imani inayojidhihirisha
katika matendo. Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Nyerere, mwanasiasa mweledi, akiongozwa
na dhamiri ya kikristo, ni mmoja wa wakristo waliotukuka katika maisha ya uadilifu
wa kisiasa na kiutu. Mtumishi wa Mungu Sr. Bernadetta Mbawala wa Shirika la Masista
Wabenediktini wa Mt. Agnes Chipole, naye alifanikiwa kuitafsiri imani katika maisha
yake na hivi akaishi maisha ya upendo unaobubujika kutoka katika imani kwa Mungu na
kwa Kanisa. Wakumbukeni hawa na wengine wengi walioishi miongoni mwetu wakimshuhudia
Kristo kwa maisha yao, tena, “iigeni imani yao” (Ebr 13:7).