Siku kuu ya Wafanyakazi ijenge na kudumisha haki jamii!
Baraza la Maaskofu Katoliki India linayataka Mashirika yanayongozwa na kusimamiwa
na Kanisa kuhakikisha kwamba, yanatoa kipaumbele cha kwanza katika kulinda na kusimamia
haki jamii; kwa kutoa mishahara inayozingatia haki pamoja na kudumisha haki msingi
za wanawake hasa wahamiaji.
Maaskofu Katoliki India katika ujumbe wao katika
Maadhimisho ya Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani Mwaka 2013 wanakazia kwamba, Kanisa
katoliki katika Mafundisho Jamii linatambua na kuthamini mchango wa vyama vya wafanyakazi
kama kielelezo cha mshikamano wa kijamii.
Majimbo na Parokia mbali mbali zimetakiwa
kuanzisha dawati litakalojadili pamoja na mambo mengine huduma za kichungaji kwa wafanyakazi
wahamiaji ili kuweza kukidhi mahitaji yao: kiroho pamoja na kuweza kuingizwa katika
maisha ya jamii inayowazunguka.
Ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanawasaidia
wafanyakazi wanaoishi katika hali duni kwa njia ya vyama vya wafanyakazi ili viweze
kuwaletea nafuu na maisha bora zaidi. Hifadhi ya jamii ni jambo ambalo kwa sasa linapewa
msukumo wa pekee na Baraza la Maaskofu Katoliki India. Maaskofu wanasema katika Maadhimisho
ya Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani kwa mwaka huu wananchi wanapaswa pia kujielekeza
katika mapambano dhidi ya ajira za watoto pamoja na kuwapatia wafanyakazi mishahara
mzuri.