2013-05-01 08:19:52

Kuweni na ari pamoja na moyo mkuu, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Lakini angalieni...!


Kardinali Mauro Piacenza, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makleri, hivi karibuni amehitimisha hija ya kichungaji nchini Poland, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa Majandokasisi na Wanovisi kutoka sehemu mbali mbali za Poland, wakionesha ile furaha ya kutaka kumfuasa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Ni vijana wenye ari na moyo mkuu ambao wako tayari kujitoa kwa furaha kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani zao kwa njia maisha na wakfu na utume wa Kipadre. RealAudioMP3

Katika mahubiri yake, Kardinali Piacenza amewaonya vijana hawa kukumbuka kwamba, ile ndiyo yao kwa Kristo na Kanisa lake halina budi kububujika kutoka katika undani wa maisha yao na wala si kwa kujisikia tu! Hili ni jibu linalogusa undani wa mtu wa kujitoa bila ya kujibakiza, hali ambayo inampatia mtu utambulisho wa kuwa kama Kristo Mchungaji mwema. Mapadre na watawa hawataweza kupata furaha ya kweli ikiwa kama wito wao hawataweza kuzamisha jibu lao katika uhalisia wa maisha kwa kushikamana na Kristo.

Vijana wanatakiwa kila wakati kufanya tafakari ya kina ili kuweza kung’amua sababu na lengo na miito yao ndani ya Kanisa kama kweli inaendana na mpango wa Kristo katika maisha yao ili waweze kufanya uamuzi wa busara badala ya kujutia maisha baadaye!

Kardinali Piacenza anawaambia vijana kwamba, ikiwa kama hawawezi kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake katika maisha ya Upadre na Utawa, wawe na ujasiri wa kusema, hapa kwa hakika maji ni mazito na hivyo kuamua kurudi nyumbani kuendelea na maisha mengine yatakayompendeza Mungu na binadamu. Kristo anapaswa kuwa ni kielelezo cha majitoleo ya hali ya juu yanayoonesha utimilifu wake kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, kwa maneno mengine majitoleo ya Kristo yanajionesha katika Msalaba.

Huu ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina kuhusu maana ya wito wa kipadre na kitawa; dhamana na wajibu wake kwa Kristo na Kanisa lake na kama kweli wako tayari kufanya hija ya Njia ya Msalaba pamoja na Kristo hadi Mlimani Kalvari, ili kuyamimina maisha yao kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu; ili kuadhimisha na kugawa Mafumbo ya Kanisa kwa watu wa Mungu.

Vijana watambue kwamba, mbele yao baada ya Upadrisho watapewa taji la miiba; mikono na miguu yao itafungwa kwa misumari. Mikono yao iliyotobolewa itaadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kuwaondolewa watu dhambi zao. Miguu yao mizito itakayokuwa inachuruzika damu, itapaswa kuwapeleka sehemu mbali mbali za dunia ili kutangaza Injili ya Kristo.

Kardinali Piacenza anabainisha kwamba, Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ni kielelezo makini cha ukuhani na ufuasi unaopaswa kutekelezwa na watoto wa Kanisa kwa njia ya sadaka na majitoleo makubwa. Ni mwaliko wa kujifunza kumwilisha fadhila za Kikristo katika maisha ya kila siku kwa kutambua kwamba: ufukara, useja na utii ni nadhiri ambazo zinapaswa kutolewa ushuhuda na Mapadre pamoja na Watawa katika ulimwengu mamboleo. Majandokasisi na Wanovisi wakati wa majiundo yao watambue na kukuza fadhila hizi zitakazokuwa ni: dira, nguzo na kielelezo cha maisha na utume wao kwa sasa na kwa siku za usoni.

Leo wao wanajiona kuwa ni Waseminari na Wanovisi, lakini kesho watapadrishwa na kuweka nadhiri zao kuwa ni Mapadre na Watawa. Watambulikane kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kama ambavyo alivyowahi kukazia Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Watambulikane katika Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa; waonekane pia katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, tayari kujimega na kujitoa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Mauro Piacenza, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makleri anasema, miaka ya malezi na majiundo ya Kipadre na Kitawa itumike vyema kwa ajili ya majiundo ya: kiakili, kiroho na kichungaji kwani mbele yao kuna changamoto nyingi zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Watambue na kujenga uhusiano na mshikamano wa dhati na Kristo na kwamba, Upadre na Utawa wao ni kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Jirani. Watafute muda wa kufanya tafakari ya kina pamoja na kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia na kuwaongoza katika wito wao wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.








All the contents on this site are copyrighted ©.