Rais Shimon Perez akutana na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 30 Aprili 2013 amekutana na kufanya mazungumzo
na Rais Shimon Peres wa Israeli, ambaye baadaye pia amekutana na ujumbe wa Viongozi
waandamizi kutoka Vatican wakiongozwa na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa
Vatican.
Katika mazungumzo haya ambayo yamefanyika katika hali ya kirafiki,
amani na utulivu mkubwa, viongozi hao wamejadili kuhusu hali ya kisiasa huko Mashariki
ya Kati na sehemu nyingine za dunia ambako bado kuna kinzani na migogoro ya kisiasa
na kijamii. Viongozi hawa wanatumaini kwamba, majadiliano kati ya Israeli na Palestina
yataanza mapema iwezekanavyo kama inavyokusudiwa kwa kuchukua hatua madhubuti, huku
wakiungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa; ili hatimaye, makubaliano yaweze kufikiwa
baina ya watu wa mataifa haya mawili, ili amani na utulivu viweze kurejea tena katika
Ukanda huo.
Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamejadili pia kuhusu Mji
wa Yerusalemu; kinzani na vita inayoendelea huko Syria na kwamba, kuna haja ya kukazia
utamaduni wa: majadiliano, upatanisho, haki na amani. Uhusiano kati ya Vatican na
Israeli, pamoja na Jumuiya za Kikristo nchini Israeli yamejadiliwa pia pamoja na kuangalia
Tume ya pamoja kati ya Israeli na Vatican na kuangalia mafanikio ambayo yamekwisha
kupatikana hadi sasa.