2013-04-30 09:15:34

Maadhimisho ya Siku ya Kuenzi Zawadi ya Uhai!


Kanisa Katoliki nchini Ireland, Jumamosi tarehe 4 Mei 2013 linaadhimisha Siku ya kuenzi zawadi ya uhai inayopania kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapokuwa bado tumboni mwa mama yake dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kauli mbiu ya Maadhimisho kwa Mwaka 2013 ni "tumbo kwa tumbo". Kitaifa siku hii itaadhimishwa kwenye Kanisa la Bikira Maria wa Knock kwa kuwashirikisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka Majimbo mbali mbali ya Ireland, ili kuombea haki ya maisha kwa watoto ambao bado hawajazaliwa; watoto ambao wanatishiwa na ukatili wa utamaduni wa kifo.

Kutokana na Serikali ya Ireland kukumbatia sheria inayoruhusu utoaji mimba, wanasema Maaskofu, watoto wengi nchini humo watakosa haki ya kuweza kuishi na kufurahia maisha ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa kuchagua kuenzi na kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, mama na mwana wote wawili wanapewa kipaumbele cha pekee.

Siku hii imetengwa na Kanisa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea akina mama na watoto wao, ili kweli wawe ni vyombo vya kuenzi zawadi ya uhai. Kanisa linawaombea ili kuwaepusha na kila ubaya; waendelee kupendwa na kuthaminiwa na wote.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linawaalika wanafamilia wote kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku hii maalum kwa ajili ya kuenzi zawadi ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Siku hii imekuwa ikiadhimishwa nchini humo tangu mwaka 2001, kama sehemu ya mchakato wa kuenzi Mafundisho ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kuhusu Injili ya Maisha "Evangelium Vitae". Mwaka 2012 waamini walitafakari kuhusu umuhimu wa mshikamano na matumaini katika Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.