Utawala bora katika ulimwengu unaobadilika ndiyo kauli mbiu iliyofanyiwa kazi na Baraza
la Kipapa la Sayansi Jamii, katika mkutano wake wa mwaka uliohitimishwa hivi karibuni
hapa mjini Vatican. Kwa namna ya pekee, wamegusia kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Jubilee
ya miaka 50 tangu Papa Yohane wa Ishirini na tatu alipochapisha Waraka wa Kichungaji,
Pacem in Terris, Amani Duniani. Wajumbe wa Baraza hili wameangalia changamoto
zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kuimarisha utawala bora.
Professa
Mary Ann Glendon, Rais wa Baraza la Kipapa la Sayansi Jamii katika hotuba yake ya
ufunguzi amezungumzia umuhimu wa siasa inayozingatia kanuni maadili katika maisha
ya mtu binafsi na jamii inayomzunguka. Uongozi ufahamike kwamba ni uwezo wa kutafuta
mafao ya wengi na kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha
mwanadamu.
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani
anabainisha kwamba, utawala bora ni kati ya mambo msingi yanayoiwezesha jamii kupata
mafao ya wengi. Ni mwaliko pia wa kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani ili
kuweza kukumbatia upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe. Watu wakijitahidi
kudumisha upendo kati yao, maendeleo yatafuata, kwani amani ni jina jipya la maendeleo
endelevu ya binadamu.
Kardinali Turkson anakazia kwamba, dhamana na wajibu
wa kujenga na kuimarisha amani ni kwa watu wote wenye mapenzi mema, changamoto kwa
kila mtu kujitahidi kuwa ni chombo cha amani na mafao ya wengi. Wajumbe hawa pia
walipata bahati ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.