2013-04-30 07:35:31

Askofu msaidizi mteule Titus Joseph Mdoe wa Jimbo kuu Dar es Salaam kuwekwa wakfu, Mei Mosi, 2013


Maaskofu kwa kuwa ni waandamizi wa Mitume wamekabidhiwa na Bwana utume wa kuyafundisha mataifa yote na kuhubiri Injili kwa kila kiumbe, ili watu wote wapate wokovu kwa njia ya imani, ubatizo na kwa kushika Amri za Mungu. Jukumu la kwanza kabisa la Askofu ni kufundisha na kutangaza imani kwa Kristo na Kanisa lake; imani ambayo inapaswa kushuhudiwa katika maisha adili. RealAudioMP3

Askofu, aliyepewa ukamilifu wa Sakramenti ya Daraja takatifu ndiye wakili wa neema ya ukuhani mkuu, hasa katika Ekaristi anayotolea mwenyewe au kuagiza itolewe, na kwa njia hiyo Kanisa daima huishi na kukua. Askofu ni ni ishara ya mapendo na umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa ambalo ni moja, takatifu, Katoliki na la Mitume.

Maaskofu kwa njia ya Sala na kazi kwa ajili ya watu, wanamimina ukamilifu wa utakatifu wa Kristo kwa namna mbali mbali na kwa wingi, lakini zaidi kwa njia ya huduma ya Neno la Mungu; Sakramenti za Kanisa na mtindo wao wa maisha.

Maaskofu wamepewa dhamana na Mama Kanisa kuyaongoza Makanisa faridi waliyokabidhiwa kama mawakili na wajumbe wa Kristo, mashauri, maonyo na mifano na uweza mtakatifu kwa ajili ya kujenga Kanisa la Kristo. Maaskofu wamekabidhiwa dhamana ya kulinda na kuchunga Kondoo wa Kristo. Wajitahidi kuwa ni wachungaji wema wanaotumikia kwa hekima na busara; wanaosikiliza, kujadili na kushauri.

Kwa ufupi haya ndiyo Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Askofu, wakati huu Mama Kanisa, Jimbo kuu la Dar es Salaam anapojiandaa kwa ajili ya kumweka wakfu Askofu mteule Titus Joseph Mdoe aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, hapo tarehe 16 Februari 2013.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule alizaliwa kunako tarehe 19 Machi 1961, Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga. Akapata elimu yake ya Sekondari kutoka Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, Morogoro. Akasoma Falsafa, kwenye Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi na kuhitimisha majiundo yake ya Kikasisi, Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Tarehe 24 Juni 1986 akapadrishwa kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Tanga.

Tangu wakati huo, amekuwa ni Paroko Msaidizi wa Parokia ya Gare, Kilole na Mkurugenzi wa Miito Jimbo Katoliki la Tanga. Aliwahi pia kuwa ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Theresa na hatimaye, kati ya Mwaka 1995 hadi mwaka 2000 akawa ni Paroko wa Hale. Mwaka 2000 hadi Mwaka 2008. Alikuwa ni Msimamizi wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Tanga.

Kati ya Mwaka 2008 hadi Mwaka 2010 alipelekwa kusoma Chuo Kikuu cha Saint Clair, huko Calfonia, Marekani, akabahatika kutapa shahada ya uzamili kuhusu shughuli za kichungaji na tasaufi. Aliporudi nchini Tanzania alipangiwa kuwa Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino cha Tanzania, SAUT, Kituo cha Stella Maris, kilichoko Jimbo Katoliki la Mtwara, Kusini mwa Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake ya kuanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alisema kwamba, madaraka ni huduma inayosimikwa katika Fumbo la Msalaba na katika Imani thabiti kama alivyokuwa Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Yesu. Ni changamoto ya kufungua mikono kwa ajili ya kuikumbatia na kuilinda Familia ya Mungu, lakini zaidi maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili wao pia waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu. Hawa ndio wale wenye njaa, kiu, wageni, walio uchi, maskini na wafungwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, yule anayehudumia kwa upendo wa dhati anatambua pia umuhimu wa kulinda.

Mtakatifu Yosefu ni mlinzi mwaminifu kwani alikuza na kudumisha ndani mwake sanaa yakusikiliza, akasoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka changamoto ya kutambua kwamba, kiini cha maisha ya Kikristo ni Kristo mwenyewe aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Kristo apewe hifadhi katika miyo ya waamini, ili nao waweze kuwahifadhi jirani pamoja na kushiriki katika mchakato wa kutunza mazingira. Mtakatifu Yosefu msimamizi wa Kanisa na Jimbo kuu la Dar es Salaam wasimamie na kuwaombea watoto wako!

Imeandaliwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.