2013-04-29 07:17:04

Pokeeni zawadi ya Roho Mtakatifu ili kumtolea Kristo ushuhuda kwa njia ya maisha!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu ambamo ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo kutoka pande mbali mbali za dunia, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili tarehe 28 Aprili 2013, aliwaweka waamini walioimarishwa kwa Mapaji ya Roho Mtakatifu chini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria wakati wa sala ya Malkia wa Mbingu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini hao kujifunza kutoka kwa Bikira Maria maana ya kuishi ndani ya Roho Mtakatifu sanjari na kuukaribisha upya wa maisha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria alitunga mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, changamoto kwa kila Mkristo kukaribisha Neno la Mungu pamoja na kumkaribisha Yesu katika maisha yake, huku akijitahidi kumpeleka kwa wengine.

Bikira Maria alikuwepo wakati wa Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume walipokuwa kwenye chumba cha juu. Baba Mtakatifu anasema, kila wakati waamini wanapokusanyika kwa ajili ya kusali wanategemezwa kwa uwepo wa Roho Mtakatifu na Bikira Maria, Mama wa Kristo, ili kuweza kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu, hatimaye, kuweza kumtolea ushuhuda Yesu Mfufuka.

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya kwa namna ya pekee akiwaelekea zaidi wale ambao wameimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anawataka wamwombe Bikira Maria ili awasaidie kuwa wasikivu kwa kile ambacho Bwana anataka kutoka kwao, daima wakijitahidi kuishi kadiri ya matakwa ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu alitambua uwepo wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Amewakumbuka na kuwaombea wakristo wote watakaopokea Sakramenti ya Kipaimara wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko ameyaelekeza mawazo na sala zake kwa watu waliofikwa na maafa ya kuangukiwa jengo la kiwanda cha kutengeneza nguo huko Dakar, Bangaladesh. Ameonesha mshikamano wake wa upendo kwa njia ya sala na familia pamoja na wote walioguswa na msiba huu mkubwa. Anaomba kutoka katika undani wa moyo wake, wahusika wote kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda utu na usalama wa wafanyakazi.

Mara baada ya Maadhimisho ya Misa takatifu na Sala ya Malkia wa mbingu, Baba Mtakatifu Francisko alizunguka Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusalimiana na waamini waliokuwa wamefurika na kujaza viunga vya Vatican, kila mmoja akiwa na hamu ya kutaka kusalimiana naye.

Baba Mtakatifu ametumia muda mrefu kidogo baada ya Misa Takatifu kusalimiana na kuzungumza na Mapadre walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, hii inaonesha moyo wa upendo na mshikamano wakidugu unaopaswa kujionesha miongoni mwa Mapadre wanapotekeleza wajibu wao kwa Kristo na Kanisa lake.








All the contents on this site are copyrighted ©.