Pokeeni mapaji ya Roho Mtakatifu ili muweze kubadilika na kuimarishwa wakati wa majaribu
na magumu ya maisha; mkishikamana na Kristo!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Pasaka, tarehe 28 Aprili
2013 ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 44 kutoka sehemu mbali mbali za dunia,
katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican, na kuhudhuriwa na bahari ya watu!
Katika mahubiri yake,
Baba Mtakatifu anasema, mbele ya Mungu mambo yote ni mapya kwani yanabadilika na kuonesha:
wema, uzuri na ukweli. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu anamwendea na kumletea
mwanadamu mabadiliko ya ndani changamoto ya kutambua kwamba, mwanadamu yuko katika
hija ya kuiendea Yerusalemu mpya, siku ambayo watabahatika kuonana na Yesu Kristo
uso kwa uso na kuishi pamoja naye milele yote katika upendo.
Baba Mtakatifu
anawaambia waamini kwamba, mambo mapya kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni tofauti kabisa
na yale yanayotolewa na walimwengu kwani mapya ya dunia ni mambo ya mpito! Roho Mtakatifu
anapowaletea waamini mabadiliko ya ndani anawataka kufanya pia mabadiliko katika ulimwengu
wanamoishi, mwaliko kwa kila mwamini kumfungulia Roho Mtakatifu mlango wa maisha yake,
ili aweze kuongozwa naye na kuendelea kupokea msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaowafanya
kuwa wapya kutokana na uvuvio wa upendo wa Mungu unaotolewa na Roho Mtakatifu.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao kila siku jioni ili kuangalia
ni kwa jinsi gani wameweza kumwilisha ndani mwao upendo wa Mungu kwa marafiki, ndugu
na jamaa au kwa wazee na wale wanaohitaji zaidi. Wakifanikiwa kutekeleza haya kwa
hakika watagundua kwamba, inapendeza.
Hija ya maisha ya Kanisa na waamini
katika ujumla wake si rahisi kwani daima imesheheni vikwazo na majaribu. Kumfuasa
Kristo ni kuruhusu Roho wake aweze kugeuza ile sura ya giza na matendo yasiyompendeza
Mungu; kuwaondolea dhambi pamoja na kuwakinga kutokana na vikwazo vinavyowazunguka
na vile ambavyo viko ndani mwa mioyo yao!
Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba,
matatizo na majaribu ya maisha ni njia inayompeleka mwamini katika utukufu wa Mungu,
kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo aliyetukuzwa na Baba yake wa mbinguni kwa njia ya
Msalaba. Vikwazo na majaribu ni sehemu ya hija ya maisha ya mwamini hapa duniani,
jambo ambalo kamwe lisiwafanye waamini kukata tamaa kwani wanayo ndani mwao ile nguvu
ya Roho Mtakatifu inayowawezesha kuyashinda yote haya!
Baba Mtakatifu kwa namna
ya pekee, amewaalika Wakristo walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kuwa imara
katika hija ya imani na matumaini kwa Yesu Kristo kwani hii ndiyo siri ya mafanikio
katika hija ya maisha ya waamini! Anawatia moyo pale wanapokumbana na mawimbi mazito
ya bahari, kiasi kwamba, wasifuate mkumbo katika maisha, kwani hili ni jambo jema
kwa ajili yao.
Wawe na ujasiri wa kukabiliana na mawimbi mazito katika maisha
yao ya kila siku, kwani Yesu mwenyewe anawakirimia ujasiri huu, ikiwa kama wataambatana
na kuendelea kuungana na Mwenyezi Mungu kwani wao ni kama matawi, ikiwa kama wataimarisha
urafiki na Mungu kwa kumpatia nafasi katika maisha yao.
Baba Mtakatifu anasema,
hili ni jambo muhimu sana kukumbuka hasa pale wanapojisikia kuwa maskini, wanyonge
na wa dhambi kwani Mwenyezi Mungu daima anawaimarisha pale wanapohisi kwamba, ni
wanyonge, anawatajirisha kutokana na umaskini wao; anawapatia toba, wongofu wa ndani
na msamaha wa dhambi. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, yuko tayari kuwasamehe watoto
wake wanapomkimbilia wakiomba msamaha, jambo la msingi, ni kujiaminisha katika kazi
ya Mungu.
Waamini wakiambatana na Mungu, kwa hakika wanaweza kufanya mambo
makubwa, kwani atawakirimia furaha ya kuwa ni wafuasi na mashahidi wake amini. Baba
Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kuwataka Waamini, lakini kwa namna ya pekee
kabisa, wale ambao wameimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kuwa na ndoto ya mambo
makubwa, kwani wamechaguliwa na Kristo kwa ajili ya mambo makubwa zaidi. Mambo mapya
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, majaribu ya maisha pamoja na kuwa imara katika Kristo ni
mambo msingi katika maisha ya mwamini.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumfungulia
Mungu malango ya maisha yao, ili waweze kupokea mapaji ya Roho Mtakatifu yanayopania
kuwabadilisha na kuwaimarisha wakati wa majaribu pamoja na kuendelea kuwaimarisha
na kushikamana na Bwana, kwani hii ndiyo furaha ya kweli!