2013-04-29 08:15:40

Parokia ni kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa Jumuiya za Kikristo


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil hivi karibuni limehitimisha mkutano wake mkuu uliokuwa unafanyika mjini Aparecida, Brazil kwa kusisitizia umuhimu wa Parokia kama kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa Jumuiya za Kikristo. RealAudioMP3

Maaskofu wamechambua pia umuhimu wa njia za mawasiliano ya jamii kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya pamoja na kupembua kwa kina na mapana sera itakayotumiwa na Kanisa katika sekta ya kilimo, ili kuinua hali ya maisha ya wananchi wengi wa Brazil.

Akizungumza na waandishi wa habari, Askofu mkuu Dimas Lara Barbosa wa Jimbo kuu la Campo Grande, amebainisha kwamba, Maaskofu waliweza kujiwekea mikakati na sera katika shughuli za kichungaji kama mwaliko wa utekelezaji wa changamoto ya Uinjilishaji Mpya katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Mikakati hii ilikwisha pitishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil na sasa ni wakati wa kuimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Odilo Scherer wakati wa Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil ameelezea kwamba, uchaguzi wa Baba Mtakatifu Francisko umeleta ari na mwamko mpya katika maisha na utume wa Kanisa. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na idadi ndogo ya waamini wa Kanisa Katoliki kadiri ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini Brazil kunako mwaka 2010. Hili ni jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa.

Hapa mwaliko ni Uinjilishaji Mpya, ili kuwajengea waamini uwezo wa kufurahia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kuiungama, kuiadhimisha, kuimwilisha na kuisali kadiri ya mwelekeo wa Kanisa. Kardinali Scherer anabainisha kwamba, haya ni mambo muhimu sana katika kutolea ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, Mama Kanisa anachangamotishwa kwa namna ya pekee kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha. Huu ni uamuzi makini ulioanzishwa na Yesu mwenyewe kwa kutambua na kuthamini utu na heshima ya kila mtu aliyekuwa ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa lijenge na kuimarisha mshikamano wa upendo na waote wanaoteseka: kiroho na kimwili.

Dhamana ya Uinjilishaji mpya ipanie kwa namna ya pekee kabisa kuwaendea Wakristo Wakatoliki ambao kwa miaka kadhaa wamesahau mlango wa Kanisa, ili kuwasaidia tena kutambua na kung’amua umuhimu wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake na kwamba, wanapaswa kuipyaisha kwa njia ya ushuhuda amini na makini. Waamini wasaidiwe kutambua umuhimu wa Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti kama njia ya kuimarisha uhusiano wao na Kristo, ili kuushuhudia kwa njia ya matendo ya huruma. Jumuiya za Kikristo ziwe ni mahali ambapo, waamini wanapendana na kushirikishana ile furaha, upendo, umoja na udugu katika imani.

Iwe ni mahali ambapo waamini wanajisikia kuwa kweli wako nyumbani. Njia mpya za mawasiliano ya Jamii, zisaidie mchakato wa Mama Kanisa katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwasiliana na umati mkubwa zaidi wa watu bila kusahau njia za kawaida kwani si waamini wote wanaopatikana kwenye mitandao ya kijamii. Maaskofu wanasema, kimsingi Kanisa linapaswa kuwa karibu na waamini wake!








All the contents on this site are copyrighted ©.