2013-04-29 10:17:20

Papa anatarajiwa kutoa hotuba ya ufunguzi wakati wa Mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia 20- 24 Mei 2013


Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi mwenye sanaa kubwa ya kusikiliza kwa makini anatambua dhamana na wajibu wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anayesimamia upendo na umoja wa Kanisa na kwamba, ameonesha utashi wa kushirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, Baba Mtakatifu pia ni Mjumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kutokana na wadhifa wake.

Ni maneno ya Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia baada ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa Juma kwa takribani saa nzima ambapo wamejadili pamoja na mambo mengine, mikakati na sera za shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika kipindi cha miaka kumi, sanjari na Makongamano ya Kitaifa kila baada ya miaka mitano.

Kwa sasa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linajielekeza zaidi katika elimu kama njia ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, Yesu Kristo akipewa kipaumbele cha kwanza kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Majiundo ya imani yawawezeshe waamini kutambua ukuu wa binadamu mintarafu Fumbo la Umwilisho; umuhimu wa Kanisa kukuza na kusimamia tunu msingi za kiutu na kimaadili; pamoja na kuendelea kutolea ushuhuda wenye kuleta mvuto kwa jamii inayowazunguka.

Kardinali Bagnasco anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kukazia umuhimu wa Kanisa kuwa karibu na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Amelipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa sera na mikakati inayopania kuwasaidia watu wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na kinzani za kisiasa na kijamii kwa sasa.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa hotuba ya ufunguzi wakati Baraza la Maaskofu Katoliki Italia litakapokutana kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 24 Mei 2013 na kwamba, Kanisa ni Jamii ya waamini ambayo daima inapaswa kuwa hai!







All the contents on this site are copyrighted ©.