2013-04-29 07:50:10

Makatekista ni wadau wakuu katika Uinjilishaji Barani Afrika


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa Kichungaji, Africae Munus, Dhamana ya Afrika, anatambua kwa namna ya pekee kabisa mchango unaotolewa na Makatekista Barani Afrika katika kuwatayarisha Wakatekumeni ili kuweza kupokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa. RealAudioMP3
Wao ni nuru inayong’aa mbele ya waamini ili kuweza kumtukuza Mwenyezi Mungu. Ni wadau wakuu wa Uinjilishaji wao waliojitoa kimasomaso kuwainjilisha ndugu zao katika Kristo.
Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa ari na moyo mkuu zaidi, Kanisa linapoadhimisha Mwaka wa Imani, Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa. Makatekista wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba, Wakatekumeni wanayafahamu walau mambo haya.
Makatekista wanapaswa kuandaliwa barabara ili waweze kutekeza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa. Majiundo haya anasema Baba Mtakatifu mstaafu hayana budi kugusa mambo ya kiakili, mafundisho tanzu ya Kanisa, Maadili na shughuli za Kichungaji pamoja na kulinda heshima na utu wa Makatekista; washughulikie mahitaji yao na familia zao, wapewe ujira au posho inayostahili.
Makatekista kwa upande wao, wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wao; watu wanaoheshimika na kuaminika katika Jamii; Wakarimu na watu wenye maadili mema. Kwani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wataweza kutoa katekesi ya kina inayomgusa Mkatekumeni katika undani wake; wataweza kuwa ni viongozi hodari wa vikundi vya sala, maadhimisho ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo pamoja na kutambua kwamba, kimsingi wao ni wasaidizi wakuu wa Mapadri kwenye Parokia na Vigango wanavyohudumia.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, anasema kwamba, huu ni utume endelevu, stahimilivu na chanzo cha uvuvio na kamwe wasijikite katika ubinafsi unaoweza kuvuruga jitihada zote hizi. Makatekista wanapaswa kuwa waaminifu katika maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuchangia kwa namna ya pekee kabisa, utakatifu wa maisha unaohitajika kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.