2013-04-29 07:26:05

Gundueni umuhimu wa kweli shirikishi za imani zinazopaswa kutolewa ushuhuda katika maisha!


Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita unaokwenda sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni fursa muafaka ya kugundua tena umuhimu wa kweli shirikishi za imani wanazopaswa kuzitolea ushuhuda amini katika uhalisia wa maisha yao ya Kikristo.

Hayo yamesemwa na Padre Kee Maas wa Shirika la Wamissionari wa Afrika wakati wa uzinduzi wa Onesho la Mwaka wa Imani, lililofanyika kwenye Kituo cha Kichungaji cha Mtakatifu Paulo, Kigali nchini Rwanda. Onesho hili lina picha ishirini na nne ambazo zimechaguliwa kama vielelezo vya Uinjilishaji nchini Rwanda mintarafu Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Porta Fidei, Mlango wa Imani.

Maelezo ya Baba Mtakatifu yameambatanishwa na picha ambazo ni mwaliko kwa waamini kufumbua macho yao ya imani ili kuweza kuona uzuri na kweli za imani shirikishi, tayari kujitosa kimasomaso kuendelea kutolea ushuhuda imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa furaha, ari na moyo mkuu zaidi.

Onesho hili la picha litatembezwa katika Majimbo yote ya Kanisa Katoliki nchini Rwanda kama njia ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na litakamilika hapo tarehe 24 Novemba 2013, katika Maadhimisho ya Sherehe za Kristo Mfalme wa Ulimwengu.

Padre Kee Maas anabainisha kwamba, imani ni mwenza wa hija ya misha hapa duniani inayomwezesha mwamini kuyaona matendo makuu ya Mungu kwa jicho jipya. Ufunguzi wa maonesho haya umehudhuriwa na Askofu mkuu Thaddèe Ntihinyurwa wa Jimbo kuu la Kigali, Rwanda pamoja na viongozi wengine wa Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.