Muswada wa sheria kuhusu "siri za Serikali" una mapungufu makubwa!
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limemwomba Rais Jacob Zuma wa Afrika
ya Kusini, kupeleka muswada wa sheria ya habari za kitaifa kwenye Mahakama ya Katiba
kabla ya kuupitisha na kuwa sheria kamili kutokana na mapungufu makubwa yaliyojionesha
kwenye muswada huo.
Ushauri huu
umetolewa na Askofu mkuu Stephen Brislin, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika
ya Kusini. Anasema, Rais Zuma ndiye mwenye mamlaka ya kuweza kuupeleka muswada huo
wa sheria kwenye Mahakama ya Katiba ili uweze kuchambuliwa vizuri zaidi kabla ya kuwekwa
sahihi na kuwa sheria ya nchi. Hii inatokana na ukweli kwamba, Wabunge wametumia muda
mwingi kuufanyia marekebisho lakini bila kupata muafaka kwa takribani miaka mitatu
sasa.
Muswada unaonesha kwamba, Serikali inayo mamlaka kudhibiti siri za Serikali,
hali ambayo wadau wengi wa mawasiliano ya jamii wanasema, kinaweza kuwa ni kichaka
cha kuficha masuala ya rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma kwa kisingizio cha
kuwa ni "siri ya serikali". Mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma
yanapaswa kuongozwa na ukweli na uwazi; ujasiri na uwajibikaji kwa ajili ya mafao
ya wengi badala ya usiri mkubwa unaoweza kukwamisha mapambano haya.
Hukumu
ya miaka 25 kwa watu watakovujisha siri za Serikali ni kubwa mno kiasi kwamba, watu
wanaotaka kukwamisha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wanaweza kuitumia sheria
hii kwa mafao ya binafsi. Wananchi wa Afrika ya Kusini wanahitaji kuwa na uhuru wa
habari.