2013-04-26 11:32:01

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yaanza kushika kasi mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko anaanza kushiriki kikamilifu matukio ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha kwa mara ya kwanza Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, mwongozo makini wa mafundisho tanzu ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 27 na Jumapili tarehe 28 Aprili 2013 anatarajiwa kukutana na umati mkubwa wa vijana watakaopokea Sakramenti ya Kipaimara au ambao tayari wamekwisha pokea Sakramenti hii katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Kilele cha tukio hili la kihistoria katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni hapo Jumapili tarehe 28 Aprili 2013, Jumapili ya tano ya Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu atakapoongoza Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 44 wanaopewa dhamana ya kwenda kumshuhudia Kristo kwa maneno na mtendo yao ya kila siku.

Kundi la Wakristo watakaoimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiwa hapa mjini Vatican watapata Katekesi ya kina kuhusu imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wataandamana na hatimaye, kukiri Imani kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, lililoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wakristo hawa wanasindikizwa na Mapadre na Makatekista wao waliowaandaa ili kuweza kushiriki katika Mafumbo ya Kanisa.

Kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Francsiko atatoa Sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo 44, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Askofu mkuu Rino Fisichella na viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, walipokuwa wanatangaza matukio makuu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Wakristo watakaoimarishwa kwa Mapaji ya Roho Mtakatifu ni wale wenye umri kati ya miaka 11 hadi miaka 55.

Askofu mkuu Rino Fisichella anaendelea kufafanua kwamba, tarehe 3 hadi 5 Mei 2013, Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, atakutana na kusali pamoja na vyama vya kitume, ambavyo vimekuwa na Ibada mbali mbali ndani ya Kanisa. Vyama hivi ni vile vinavyotoka kwenye nchi ambazo zina utamaduni wa muda mrefu. Wanachama watakuwa na fursa ya kutolea ushuhuda wa imani yao inayojionesha pia katika sanaa kwa miaka mingi. Itakuwa ni nafasi kwa wanachama hawa kusali Rozari Takatifu na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, tarehe 4 Mei 2013, Saa 12:00 jioni.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na wanachama wa Mashirika haya, Jumapili tarehe 5 Mei 2013, kuanzia saa 4:00 Asubuhi. Haya ni matukio yanayofumbatwa katika hija ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Ni kielelezo cha Mapokeo ya Imani ambayo yamerithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine ndani ya Kanisa. Haya ndiyo matukio yanayopaswa kushuhudiwa katika Imani, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; Kuyamwilisha katika maisha adili na kuyasali kwa ujasiri, ibada na moyo mkuu.







All the contents on this site are copyrighted ©.