UN: tekelezeni wajibu wenu ili kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria
Viongozi wa Jumuiya ya Kimatafa kunako mwaka 2000 walijiwekea Malengo ya Maendeleo
ya Millenia ifikapo mwaka 2015; mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria na Ukimwi ni
kati ya malengo hayo.
Kuna baadhi ya nchi ambazo zimeonesha mafanikio makubwa
katika kupambana na ugonjwa wa Malaria kwa kuboresha huduma za afya, uchunguzi wa
magonjwa, matumizi ya vyandarua vvyenye dawa sanjari na matumizi ya dawa sahihi ni
kati ya mambo ambayo yamesaidia kupunguza vifo vya mamillioni ya wagonjwa wa Malaria
duniani.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon katika ujumbe wake
kwa Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2013 anabainisha kwamba, licha ya jitihada zote
hizi lakini, Malaria bado ni ugonjwa unaoendelea kusababisha vifo vya watu wengi duniani;
na kwa namna ya pekee Barani Afrika.
Hii inatokana na ukweli kwamba, hakuna
taarifa rasmi za ugonjwa wa Malaria; kuna baadhi ya maeneo ambayo wadudu wa Malaria
wamekuwa sugu pamoja na matumizi hafifu ya vyandarua. Haya ni mambo ambayo yanakwamisha
juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Licha ya wadau kuchangia katika Mfuko
wa Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa malaria, lakini bado kuna pungufu ya dolla za kimarekani
billioni 3.
Kuna nchi kumi ambazo ugonjwa wa Malaria umeendelea kuwa sugu
na chanzo kikuu cha vifo vya watu wake. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha
kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inawajibu wa kuchangia mapambano dhidi ya ugonjwa wa
Malaria katika nchi hizi ili kuokoa maisha ya watu. Juhudi hizi hazina budi kwenda
sanjari na mapambano dhidi ya Ukimwi na Kifua Kikuu duniani. Kampeni ya maadhimisho
ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2013 ni wekeza katika siku za usoni. Shinda Malaria.
Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria yanapania
si tu katika kuboresha afya ya watu, bali ni sehemu ya mchakato wa kujenga jamii ya
kimataifa yenye afya bora, changamoto kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza
ahadi zao katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria, kwani huu ni ugonjwa ambao
watu wanaweza kujikinga wasiugue!