2013-04-25 07:57:55

Maendeleo ya SAUT ni jeuri ya watanzania kutaka kujitegemea!


Mheshimiwa Padre Charles Kitima, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania, SAUT katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba sera ya kujigemea inapania kukuza na kuendeleza mafanikio yaliyokwisha kupatikana. RealAudioMP3

SAUT inatoa kipaumbele cha kwanza katika kuandaa rasilimali watu watakaoshiriki kwa namna ya pekee katika mikakati ya uongozi na ufundishaji. Hawa ni watu wanaoteuliwa kutokana na sifa zao: watu wenye mwono na dira sahihi; weledi, wenye ari na moyo wa kutaka kuwahudumia watanzania kadiri ya malengo na sera za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Padre Charles Kitima anasema ni kweli kwamba, rasilimali fedha na vifaa vinahitajika sana, lakini jambo la msingi ni kuwekeza katika rasilimali watu, kwa kuwajengea uwezo wa kuibua sera na mikakati ya kujitegemea na kukitegemeza Chuo; watu wenye uchungu na kiu ya kutaka maendeleo ya wengi; watu wenye moyo wa kujituma na sadaka. Hawa ni watu wanaopaswa kuwa na nidhamu ya matumizi sahihi ya bajeti ya Chuo. Ili kujitegemea, SAUT inaendelea kuboresha kiwango cha elimu ili kupata wanafunzi wengi zaidi.

Padre Kitima anakiri kwamba, SAUT kwa sasa kinaweza kujitegemea kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kuwa na matumizi bora ya rasilimali watu na fedha iliyopo. Misaada kutoka kwa wahisani na wadau mbali mbali wa elimu inachangia katika maboresho ya miundo mbinu. Lakini anakumbusha kwamba, kiwango cha misaada kwa sasa ni kidogo sana. Mikakati ya kujitegemea SAUt inajikita katika jeuri ya watanzania kwa kuangalia uchumi wake.

SAUT ilianza ikiwa na wanafunzi 294, lakini leo hii ni kati ya Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Barani Afrika vyenye idadi kubwa ya wanafunzi. SAUT inaendelea kushikamana na Vyuo Vikuu vya Kikatoliki ili kushirikishana ujuzi, uzoefu na mang'amuzi mbali mbali katika mchakato wa kuliwezesha Kanisa Barani Afrika liendelee kuinjilisha kwa njia ya sekta ya elimu inayojali mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Padre Charles Kitima anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu wanaoendelea kukiunga mkono Chuo Kikuu cha SAUT kwa kutoa rasilimali watu, fedha na ushauri kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya SAUT Tanzania na katika Bara la Afrika kwa ujumla.







All the contents on this site are copyrighted ©.