Jengeni urafiki na Yesu kwa Njia ya: Sala, Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti
“Siwaiti tena watumishi bali nawaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba
yangu nimewaarifu”. Haya ni maneno ya Kristu kwa wafuasi wake, lakini maneno haya
yanalia leo masikioni mwako kijana na yana uzito na umuhimu ule ule. Wewe ni rafiki
wa Kristo, ndivyo anavyokutambua. Kazi kwako kujiuliza je, wewe ni mwaminfu kiasi
gani katika urafiki huo. Labda kabla ya
kufika katika swali hilo, jiulize kwanza kama wewe mwenyewe unajitambua hivyo na kumkubali.
Karibu sana ndugu msikilizaji katika hema letu vijana leo. Chukua nafasi yako na kwa
furaha kabisa na uelewa wa kirafiki tutafakari pamoja juu ya urafiki wetu na Kristo. Tuanze
kwa kuona tabia na kisha umuhimu wa rafiki katika maisha. Rafiki ni mtu aliye karibu
nawe. Ukaribu huu sio ukaribu wa ujirani, bali ni ukaribu wa mahusiano. Kumbe yawezekana
kabisa ukawa mbali sana na mtu huyo lakini yeye bado ni rafiki yako kipenzi. Kumbe,
umbali hauvunji urafiki. Urafiki unakuwepo na udumu kwa ule ukaribu wa ndani uliopo
kati yako na rafiki yako. Rafiki hatambuliki kwa ukaribu wa kijirani bali rafiki wa
kweli hujulikana wakati wa shida. Rafiki ni mtu mwenye kukupenda. Upendo ni hisia
za ndani ambazo hazipimiki kwa urahisi. Ni wazi kwamba unaweza kutambua upendo wa
mtu kwa namna anavyokusalimu, kwa namna anavyokuchukulia, kwa namna anavyokutendea.
Kumbe kuna ishara za nje zinazoweza kuashiria upendo wa mtu. Hata hivyo, napenda uchukue
tahadhari katika hili. Wengi wanaweza kuonesha ishara za nje za wazi kana kwamba wanakupenda
lakini ndani mwao wana masilahi binafsi. Watu wa namna hii wakishapata wanachohitaji
au kufikia malengo yao hutaona tena upendo wao. Kumbe, zingatia zaidi hisia za
ndani zaidi na ishara nyingi za kudumu zinazoendana na upendo huo. Tambua pia kuwa
rafiki hujitahidi kuishi kadiri ya hali halisi. Mkiishi vitu vya kujilazimisha sana
eti kuoneshana upendo inabidi muwekane sawa juu ya uhalisia wa urafiki wenu. Rafiki
ni mkweli na muwazi kwako. Kawaida marafiki huongea mara kwa mara na kuelezana ukweli.
Ukweli na uwazi ni kujifunua kwa mwenzio, kujitambulisha wazi jinsi ulivyo bila kufichaficha.
Mahusiano ya kweli, si ya ulaghai na unafiki. Katika hali hiyo marafiki hukosoana
na kurekebishana kwa upendo. Urafiki wa kweli hauendekezi ushindani usio na msingi. Kudumu
katika mahusiano ya karibu ni sehemu ya tabia ya urafiki. Inawezekana mkawa mbali
lakini mnawasiliana mara kwa mara. Hapa uwe makini kidogo. Ile mara kwa mara inategemea
na njia za mawasiliano, muda wa kila mmoja, hali zenu kiuchumi, kijamii, kisiasa na
kadhalika. Yote haya huathiri mawasiliano. Pamoja na hayo, jiulize je, unaweka kipaumbele
kiasi gani katika kuwasiliana na rafiki yako? Uwepo kifizikia pia ni muhimu katika
urafiki. Hata pamoja na umbali. Basi, yafaa kutafuta nafasi kadha wa kadha ili kuonana.
Uwepo wa rafiki si lazima kuwa na maongezi marefu na porojo zisizo na mipaka. Mnaweza
kukutana na kuwa pamoja, kwa maongezi machache. Mara nyingine unaweza ukawa unahitaji
tu uwepo wa rafiki bila kusema neno. Kuonana katika hali ya ukimya na utulivu lakini
ukafaidika na faraja kutoka kwa rafiki yako. Duh!, Ee Bwana weee! Unaelewa kadiri
ninavyoongea kuhusu urafiki naona ninachana tu mistari na dakika zinayoyoma. Sasa
ni vizuri tuwakane sawa mapema. Hayo tuliyojadiri kuhsu urafiki, kwa kweli ndivyo
Kristo anakuhitaji wewe kijana uwe kwake. Yeye anakupenda na kukuamini, anapenda wewe
pia umpende na kumwamini. Kashuka na kuishi katika hali ya kibinadamu ili awe karibu
nawe, naye amebaki nawe katika s Sakramenti mbali mbali na hasa katika Ekaristi
Takatifu. Kristo anapenda kuonana nawe katika Sakramenti hizo. Kutana na rafiki yako
katika Ubatizo, Kitubio, ndoa na kadhalika. Jiweke katika hali nzuri kupokea Ekaristi
Takatifu uishi na kudumu naye. Chukua muda kila unapoweza, walau mara moja kwa juma,
ukae mbele ya Yesu wa Ekaristi katika utulivu na kumwabudu. Mweleze Kristu shida
zako, kuwa wazi kwake. Sali kwa bidii, ongea naye katika Neno lake, soma Injili Takatifu,
Itafakari na Kuimwilishwa katika maisha. Usimwogope rafiki yako, huna sababu ya kumwogopa
bali yafaa umpende na kumkaribia. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, mwaka
2005 alikwambia “usimwogope Kristo, maana yeye hachukui chochote kutoka kwako, badala
yake ukimpokea na kudumu naye anakupa kila kitu” Tuonane tena juma lijalo. Kutoka
Studio za Radio Vatican, ni sauti ya kinabii, Padre Celestine Nyanda.