"Huyo ni mimi ... tangu kutungwa mimba tumboni mwa mama yangu"
Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania lilizindua kampeni ya zawadi ya
maisha kwa mwaka 2013, inayoongozwa na kauli mbiu "Huyo ni mimi... tangu kutungwa
mimba tumboni mwa mama yangu" inayopania kuwahamasisha waamini na watu wote wenye
mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto
anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya
mpango wa Mungu.
Kampeni hii inawajumuisha watu mbali mbali ambao kwa hiyari
yao wenyewe wameamua kutoa picha za watoto, ndugu na jamaa katika umri mbali mbali
ili kuonesha ukuaji wa mtu, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi
mauti inapomfika. Watu wanaelezea umuhimu wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea
kushika kasi sehemu mbali mbali za dunia.
Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania
linabainisha kwamba, Kanisa linapenda kusherehekea zawadi ya maisha, tangu pale mtoto
anapotungwa mimba, kwani maisha ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Wazazi wana
wajibu wa kwanza kabisa wa kulinda watoto ambao bado wangali tumboni mwa mama zao
dhidi ya vitisho na sera za utoaji mimba. Kwa kuthamini Injili ya Uhai, watu wataweza
kuwa na ujasiri wa kutetea maisha ya watu wengine sehemu mbali mbali za dunia.