2013-04-25 08:31:58

Baada ya miaka 35, watoto nchini Somalia waanza kupata chanjo ya kuzuia magonjwa!


Serikali ya Somalia kwa kushirikiana na wadu mbali mbali imeanza kutoa chanjo itakayosaidia kuwakinga watoto wenye umri chini ya miaka mitano na magonjwa mbali mbali yanayoweza kuzuilika kwa njia ya chanjo. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, Somalia ni kati ya nchi ambazo zina idadi kubwa ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano.

Serikali ya Somalia imejiwekea lengo kwa mwaka 2013 kutoa chanjo kwa watoto 425, 000 wenye umri chini ya mwaka mmoja. Itakumbukwa kwamba, Somalia imeathirika kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imedumu kwa takribani miaka 20, jambo ambalo limekwamisha maendeleo katika sekta ya afya, hususan chanjo kwa watoto wadogo. Kutokana na hali hii kuwa mbaya, wadau mbali mbali wameahidi kugharimia chanjo kwa watoto wadogo hadi kufikia mwaka 2016.

Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa nchini Somalia linawahamasisha wazazi, viongozi wa Serikali na kidini kuunga mkono kampeni hii kwa ajili ya mafao ya watoto hawa ambao ni tegemeo la Somalia kwa siku za usoni. Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 35 watoto wa Somalia wanapata tena fursa ya kupewa chanjo dhidi ya magonjwa mbali mbali, hali ambayo imechangia pia ongezeko la vifo vya watoto wadogo nchini Somalia.

Kampeni hii inaungwa mkono pia na Shirika la Afya Duniani pamoja na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa ili kuwakinga watoto wadogo nchini Somalia wanaokabiliwa na vifo kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiliwa kwa njia ya chanjo.







All the contents on this site are copyrighted ©.