Msilegeze kamba Malaria bado inapukutisha maisha ya watu Barani Afrika
Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2013, Bara la
Afrika linapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutambua kwamba, bado kuna asilimia 33%
ya vifo Barani Afrika vinavyosababishwa na ugonjwa wa Malaria, kadiri ya taarifa ya
Malaria Duniani kwa Mwaka 2012.
Mikakati ya mapambano dhidi ya Malaria imepelekea
kuokoa maisha ya watu millioni 1.1. Bado kuna idadi kubwa ya watoto wanaopoteza maisha
yao kutokana na Malaria Barani Afrika, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa kamwe.
Dr.
Luis Sambo, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika anabainisha kwamba,
kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2013: Wekeza katika
siku za usoni. Shinda Malaria inakwenda sanjari na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo
ya Millenia ifikapo mwaka 2015.
Huu ni mwaliko kwa wadau mbali mbali kuchangia
kwa hali na mali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria Duniani pamoja na kuwa
na sera makini dhidi ya Malaria bila kusahau kujenga na kuimarisha ushirikiano wa
dhati. Utamaduni wa usafi wa mazingira, matumizi sahihi ya vyandarua na dawa pamoja
na kuendeleza tafiti zitakazosaidia kufutilia mbali ugonjwa wa Malaria ni kati ya
mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya Malaria
Duniani.