Mikakati ya SAUT katika maboresho ya elimu nchini Tanzania
Kanisa Katoliki nchini Tanzania ni kati ya wadau wakuu wa sekta ya elimu. Kanisa limekuwa
likichangia kwa namna ya pekee katika maboresho ya elimu yanayolenga kuwajengea wanafunzi
uwezo wa kupambana na mazingira yao, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa
kuishi.
Familia zenye
uwezo wa chini zimekuwa zikipewa kipaumbele cha pekee katika mikakati ya elimu inayotolewa
na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Katika mahojiano na Radio Vatican,
Mheshimiwa Padre Charles Kitima, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino
cha Tanzania, SAUT anapembua baadhi ya mikakati inayotekelezwa na SAUT katika maboresho
ya elimu ya juu nchini Tanzania. Anasema, mkakati wa kwanza unapania kuwaandaa wahadhiri
wenye upeo, moyo na ari ya kuweza kuwahudumia watanzania mintarafu sera na malengo
ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Hadi sasa SAUT ina wahadhiri wapatao
1,000 wanaotekeleza majukumu yao kwenye Matawi 11 ya SAUT yaliyoenea sehemu mbali
mbali za Tanzania. SAUT inapenda kuona kwamba, wahadhiri wote wanaofundisha SAUT wanafikia
kiwango cha shahada ya uzamivu.
Hii ndiyo maana SAUT inaendelea kuwekeza sana
katika mkakati huu ili kuboresha kiwango cha elimu nchini Tanzania na wale wanaopikwa
hapo wawe wameiva barabara tayari kujimwaga uwanjani kuwahudumia watanzania.
Kwa
miaka kumi hivi, SAUT imeendelea kuwa na kiwango cha chini ya ada ikilinganishwa na
Vyuo vingine nchini Tanzania. Lengo ni kuwajengea watanzania utamaduni wa kulipa,
kwa kujinyima na kwa njia ya sadaka, ili kuwapatia watoto wao fursa ya elimu ya juu
kwani elimu ni mkombozi. Kutokana na sera hii, SAUT imeendelea kuwa na idadi kubwa
ya wanafunzi wanaojiunga na Chuo Kikuu hiki.
Kuna jumla ya wanafunzi 28,000
kutoka SAUT na CUHAS, yaani Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afya ba Sayansi Mwambata
Bugando. Padre Charles Kitima anasema kwamba, Kanisa Katoliki Tanzania linahudumia
wanafunzi wote hawa katika Vyuo vyake vikuu na huu ni mchango mkubwa kwa Jamii ya
Watanzania na kwamba ada wanayotoza inalipika.
SAUT imeamua kutumia vigezo
vya juu wakati wa kudahili wanafunzi wanaotaka kujiunga na SAUT, lengo ni kuwa na
kiwango cha juu cha elimu ili wanafunzi wanaotoka SAUT wawe na viwango stahiki tayari
kukabiliana na soko la ajira ndani na nje ya nchi.