Imani hai inajidhihirisha katika matumaini na mapendo
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea
kukushirikisha barua ya kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Maaskofu wanasema, Imani hai inajidhihirisha
katika matumaini na mapendo. Wanajadili pia changamoto mbali mbali ambazo Wakatoliki
Tanzania wanakumbana nazo. Kutujuza zaidi ndani ya viunga vya Radio Vatican ni Sr.
Gisela Upendo Msuya.
Imani ya kweli
inajidhihirisha katika matumaini na upendo. Fadhila hizi tatu za kimungu haziachani
(Rej. 1Kor 13:13). Upendo, kama anavyoandika Mt. Agostino, kwa kawaida unatanguliwa
na imani: “Upendo kwa Mungu na kwa jirani utatoka wapi bila imani? Anawezaje mtu kumpenda
Mungu asiyemwamini?” Imani ni ufunguo unaotuingiza katika mji wa Mungu, mji ambao
wale wanaoishi ndani yake, wanatembea kwa miguu ya matumaini na upendo. Imani ya kweli
ni lazima ijidhihirishe kwa kukua katika matendo ya upendo (Rej. Yak 2:14-18 ).
Huu
ni ushuhuda wa upendo, unaojenga imani na kuikuza imani. “Imani inakua pale inapotiwa
katika maisha kama uzoefu wa upendo uliopokelewa na pale inaposhirikishwa kwa wengine
kama uzoefu wa neema na furaha. Inatufanya kuzaa matunda, kwa sababu inapanua ndani
ya mioyo yetu matumaini na kutuwezesha kuwa na ushuhuda ulio hai: hakika, inafungua
mioyo na akili za wale wanaosikiliza kuuitikia mwaliko wa Bwana wa kushikilia neno
lake wa kuwa wafuasi wake.” Imani pia inajenga matumaini na matumaini ni dhihirisho
la kile tunachokiamini. Kwa hiyo Mwaka wa Imani ni mwaliko pia wa kukua katika fadhila
hizi za kimungu.
Changamoto mbali mbali hasa za mahusiano na watu wa Jumuiya
nyingine za Kikristo na dini nyingine.
Kama Wakristo Wakatoliki wa Tanzania
tunaiishi imani yetu tukiwa katika jamii iliyo pia na watu wenye imani tofauti na
imani yetu. Kati ya hawa wapo wanaoamini baadhi ya yale tunayoamini na wengine ambao
hawaamini kabisa kile tunachokiamini. Pamoja na tofauti zetu za kiimani, Kanisa Katoliki
linaamini katika uhuru wa kuabudu na linaheshimu watu wa dini na madhehebu yote. Kwa
kuzingatia ukweli huo, Kanisa limejitahidi sana kuunda mazingira ya mazungumzano kati
yake na wakristo wa madhehebu mengine na watu wa dini nyingine kwa lengo la kukuza
mshikamano, kuheshimiana na kuelekeza nguvu zetu katika kudumisha utu wa binadamu
na amani ya Taifa letu.
Katika siku za karibuni yamejitokeza matukio yasiyopendeza
na ya kusikitisha. Kashfa dhidi ya dini na madhehebu mengine zinazidi kuendelea na
hali hiyo inaanza kuonekana kuwa ni utamaduni usio rasmi wa Taifa letu kwa sababu
unafumbiwa macho. Yamekuwepo matukio ya kuchomwa moto kwa nyumba za ibada na baadhi
ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini kutumika kuanzisha na kuendeleza
malumbano, uchochezi, chokochoko na kashfa za kidini. Hali hii haijengi na ni kukosa
heshima kwa imani za wengine. Kanisa linaamini kwa dhati kabisa kuwa, “Katika matumizi
ya uhuru wowote, watu lazima waheshimu kanuni ya kimaadili ya uwajibikaji wa binafsi
na wa kijamii.” Kama Kanisa Katoliki nchini tunawaomba waamini wetu msishawishike
kutenda jambo lolote kinyume na maelekezo ya upendo wa kiinjili. Kuweni macho mkidumu
katika sala. Kuweni wapole kama hua, lakini wenye busara kama nyoka (rej. Mt 10:16).
Tunaomba msitumie muda wenu kuhubiri juu ya imani zisizowahusu. Jikiteni katika kuijua
na kuiishi imani yetu kwa kina. Lakini pia tunaziomba mamlaka kuu kutoruhusu kujengeka
utamaduni wa kusia mbegu za chuki na migongano inayoteteresha imani. Tusikubali kufika
mahali ambapo matukio yasiyo ya kawaida yakaonekana kuwa ni ya kawaida, hasa yanapoendelea
kutokea na nguvu za dola zikaonekana kuwa kimya au kuzidiwa nguvu.