Jumuiya ya Kimataifa yasikitishwa na mauaji ya watu 187 nchini Nigeria
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amesikitishwa na taarifa ya vifo
vya watu 187 vilivyotokea nchini Nigeria, baada ya mapambano makali kati ya Jeshi
la Serikali na Kikundi cha Boko Haram yaliyotokea mwishoni mwa Juma, huko Kaskazini
Mashariki mwa Nigeria.
Katibu mkuu anasema hakuna sababu yoyote ile ya kimsingi
inayoweza kuhalalisha mauaji ya watu hawa. Kila upande unaohusika unawajibika kulinda
na kudumisha haki msingi za binadamu pamoja na kulinda maisha ya raia.
Rais
Goodluck Jonathan wa Nigeria ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo kufanya
uchunguzi wa kina kuhusiana na mauaji ya raia. Anaendelea kusubiri taarifa ya Tume
aliyounda ili kuangalia uwezekano wa kutoa msamaha kwa wana mgambo wa Boko Haram ambao
wamekuwa ni tishio kwa usalama na maisha ya wananchi wa Nigeria. Taarifa zinaonesha
kwamba, Boko Haram hawana mpango wa kufanya mazungumzo na Serikali ya Nigeria.