2013-04-22 10:52:59

Wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Roma wapewa uraia wa heshima!


Katika Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 2,766 tangu Mji wa Roma ulipoanzishwa, Mstahiki Meya Gianni Alemanno wa Jiji la Roma, ameamua kwamba, wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko Jijini Roma, yaani: Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuendeleza Kilimo na Chakula IFAD, wamepewa uraia wa heshima mjini Roma.

Mstahiki Meya Alemanno amepongeza juhudi zinazofanywa na mashirika haya matatu ya Umoja wa Mataifa katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini sehemu mbali mbali za dunia; pamoja na kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula sanjari na kuendelea kuboresha hali ya maisha ya watu wanaoishi vijijini.

Kwa upande wake Bwana Josè Graziano da Silva mkurugenzi mkuu wa FAO akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko Roma ameushukuru uongozi wa Jiji la Roma kwa kuwapatia heshima hii na kwamba, wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wamekuwa wakiungwa mkono na uongozi wa Jiji la Roma. Kwa njia ya mshikamano wa Kimataifa, wanapania kwa namna ya pekee kutokomeza baa la njaa na utapiamlo pamoja na na umaskini.







All the contents on this site are copyrighted ©.