2013-04-22 10:16:24

Umaskini bado unatishia maisha Kusini mwa Jangwa la Sahara


Taarifa ya Benki ya Dunia inaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka thelathini iliyopita, kumekuwepo na maboresho makubwa ya hali ya maisha ya watu wengi duniani, kiasi kwamba, kiwango cha umaskini katika ngazi ya dunia kimepungua kwa kiasi fulani, lakini hakuna haja ya kujigamba bali kuendelea kuweka mikakati ili kufanikisha mchakato wa kupunguza kama siyo kufuta kabisa umaskini duniani. Idadi ya watu wanaolazimika kuishi kwa kiwango cha dolla moja na senti ishirini na tano ya Kimarekani kwa siku, imeshuka kwa asilimia 50% tangu mwaka 1981 hadi kufikia asilimia 21% kwa mwaka 2010.

Benki ya Dunia inabainisha kwamba, kiwango cha umaskini kinaweza kuwa kimepungua kwa ujumla lakini bado kuna baadhi ya nchi ambazo watu wake wanaishi katika umaskini mkubwa. Hali hii inajionesha kwa namna ya pekee, Kusini mwa Jangwa la Sahara, sehemu ambako idadi ya kiwango cha umaskini imeongezeka tangu mwaka 1981 hadi sasa, jambo ambalo linaonesha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa bado inakabiliwa na changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya baa la umaskini kama anavyobainisha Bwana Jim Jong Kim, Rais wa Benki ya Dunia, wakati wa uzinduzi wa taarifa hii hivi karibuni.

Anasema, kuna zaidi ya watu billioni moja wanaoendelea kuishi katika umaskini wa kipato, changamoto kwa kila mtu kuhakikisha kwamba, anatekeleza wajibu wake katika mchakato wa kupambana na baa la umaskini duniani. Takwimu za Benki ya Dunia zitoe changamoto chanya kwa Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo kujifunga kibwebwe ili kupambana na baa la umaskini wa kipato ifikapo mwaka 2030.

Taarifa hii ineonesha mahali ambapo kuna kiwango kikubwa cha umaskini na jinsi ambavyo maskini hao wanavyochakarika kupambana na umaskini wao!








All the contents on this site are copyrighted ©.