Mshikamano wa kidugu na waathirika wa vita Mashariki mwa DRC
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo imetoa dhamana kwa Shirika la
Misaada la Kanisa Katoliki Caritas DRC kusimamia na kugawa msaada wa mshikamano wa
kitaifa kwa watu walioathirika na vita Mashariki mwa DRC. Kampeni hii ya mshikamano
wa kidugu kitaifa inatarajiwa kudumu walau kwa muda wa miezi mitatu na imezinduliwa
hivi karibuni na Bwana Charles Naweji, Waziri wa Jamii, misaada na mshikamano wa kitaifa.
Hii inatokana na ombi lililotolewa na wadau mbali mbali wa misaada ya kijamii
kutoka ndani na nje ya DRC kutaka dhamana ya kusimamia na kugawa misaada ya mshikamano
wa kitaifa wapewe Caritas DRC. Wananchi na watu wenye mapenzi mema ndani na nje ya
DRC kwa namna ya pekee wanaalikwa kuonesha mshikamano wa kidugu na wananchi wa DRC
wanaoishi Mashariki, ambayo kwa takribani miaka ishirini wameendelea kuathirika kutokana
na vita inayorindima sehemu hizo.
Shirika la Habari za Kimissionari FIDES linabainisha
kwamba, kampeni ya mshikamano wa kitaifa inaendeshwa na Mashirika ya Kitawa, Mashirika
Yasiokuwa ya Kiserikali na Watu binafsi ambao watapita sehemu mbali mbali za DRC kuomba
na kukusanya misaada kwa ajili ya waathirika wa vita Mashariki mwa DRC.