2013-04-19 10:41:23

Mwanahabari bora wa Mwaka 2013 ni P. Lombardi


Padre Federico Lombardi, SJ. Msemaji mkuu wa Vatican na Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican, Alhamisi tarehe 18 Aprili 2013 amepewa tuzo la kuwa ni Mwanahabari Bora wa Mwaka na Kampuni ya Allianz baada ya kuchaguliwa na Wakurugenzi wakuu wa Taasisi hii ya habari inayotekeleza majukumu yake kwenye nchi 70 na inawafanyakazi wapatao 150, 000 na inahudumia wateja zaidi ya millioni 76.

Kampuni hii imemtaja Padre Federico Lombardi kuwa ni mtu mwenye mawazo na msimamo thabiti; mwanahabari anayeonesha utulivu wa ndani na uhakika wa kile anachozungumza. Ni mtu mwenye uwezo mpana wa kukabiliana na hali ngumu ya kazi, lakini daima anagusa na kufafanua undani wa mambo bila kupindisha ukweli. Padre Lombardi ni ufunguo makini wa kutambua na kufahamu matukio mbali mbali yanayoendelea mjini Vatican.

Ni kiongozi mwenye upeo mkubwa, mang'amuzi na weledi wa muda mrefu katika shughuli zake. Sifa hizi zote zinampatia haki ya kupewa tuzo la kuwa ni mwanahabari bora kwa mwaka 2013. Ni mwalimu wa uelewa na uhakika wa mambo na kamwe hafanyi kazi zake kwa kubahatisha.

Tuzo hii amekabidhiwa Padre Lombardi kama sehemu ya Maadhimisho ya Kongamano la Mwaka lililofanywa na Kampuni hii kwa kujikita katika mawasiliano. Hafla hii fupi imehudhiriwa na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na wageni wengine mashuhuri kutoka ndani na nje ya Vatican.

Padre Lombardi katika kongamano hili amepembua kwa kina na mapana kazi na shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na Idara ya Habari ya Vatican, kwamba, lengo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, inasaidia kutoa habari za ukweli mintarafu mfumo wa mawasiliano wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna njia mpya za mawasiliano zinazomgusa mtu moja kwa moja na kwa njia ya haraka.

Jambo hili linapendeza na huu ndio mwelekeo mpya wa mawasiliano ya Kijamii yanayogusa kwa namna ya pekee kipaji cha ugunduzi na majitoleo. Padre Lombardi anasema, kuna haja ya mtu kuipenda, kuithamini na kuitafsiri kazi hii katika huduma makini kwa wale wanaohitaji. Radio Vatican inampongeza kwa umakini mkubwa anapotekeleza wajibu na dhamana yake katika sekta ya mawasiliano ya Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.