Msamaha unaweza kutolewa kwa Kikundi cha Boko Haram ikiwa kama watatubu pamoja na
kulipa fidia waathirika wa vitendo vya kigaidi walivyotenda!
Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ameunda Tume ya watu ishirini na sita, ili kuanzisha
mchakato wa majadiliano kati ya Serikali na Kikundi cha Boko Haram, ili kuweza kufikia
muafaka wa amani na utulivu, Kaskazini mwa Nigeria, sehemu ambayo kwa miezi kadhaa
imekuwa ni uwanja wa mashambulizi na mauaji ya kujitoa mhanga.
Tume hii imepewa
jukumu la kutafuta mbinu zitakazotumiwa na Serikali ili kutoa msamaha kwa wahusika
wa Kikundi cha Boko Haram, sanjari na kusalimisha silaha katika kipindi cha siku 60.
Tume pia itatoa mapendekezo ya jinsi gani waathirika wa vitendo haramu vilivyofanywa
na Kikundi cha Boko Haram watakavyosaidiwa.
Tume hii inaongozwa na Waziri asiyekuwa
na Wizara maalum Bwana Kabiru Tanimu Turaki na kuwajumuisha wajumbe kutoka katika
dini, wabunge, wanajeshi, wasomi, wanasheria, wanadiplomasia na watetezi wa haki msingi
za binadamu.
Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2009 zaidi
ya watu 1,500 waliuwawa kikatili na Kikundi cha Boko Haram, ambacho kilijielekeza
katika kuyashambulia Makanisa na Waamini waliokuwa Makanisani. Hivi karibuni, Kamanda
mkuu wa Kikundi hiki Bwana Abubakar Shekau alikanusha jitihada za kutaka kuwapatia
msamaha. Bado mashambulizi na madhulumu ya kidini yanaendelea nchini Nigeria watu
wasiokuwa na hatia wanauwawa kinyama na makazi yao kuchomwa moto.
Kardinali
John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nigeria anabainisha kwamba,
kutoa msamaha kwa Kikundi cha Boko Haram inawezekana kuwa ni moja ya njia ya kusimamisha
mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia.
Katika vita, kuna wakati inawabidi
wahusika wakuu kukaa chini kitako na kuanza kujadili uwezekano wa kupata ufumbuzi
wa mgogoro wao, bila shaka hiki ni kipindi maalum cha kujadiliana na Boko Haram, kwani
ni vyema zaidi kufanya majadiliano kuliko kuachilia mtutu wa bunduki kuendelea kurindima
na hivyo kufyeka maisha ya watu wasiokuwa na hatia.
Kardinali Onaiyekan anasikitika
kusema kwamba, kutoa msamaha kwa Kikundi cha Boko Haram bila wao wenyewe kutambua
makosa waliyowatendea wananchi wa Nigeria kwa kusababisha mauaji makubwa na uharibifu
wa mali ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa! Kikundi cha Boko Haram kinapaswa kutubu na
kukiri makosa yao; wawajibishwe kulipa fidia kwa waathirika wa vitendo vya kigaidi
walivyoendesha. Masharti haya mawili yakitekelezwa, msamaha unaweza kutolewa na haki
kutendeka, kwani haki na msamaha ni chanda na pete.