Ni siku nyingine tena tunakutana katika kushirikishana Neno la Mungu Neno ambalo ni
kiunganishi cha maisha kati yetu na Baba wa mbinguni. Tunaendelea katika safari ya
furaha ya Pasaka, tayari tuko Dominika ya IV ya Pasaka.
Kama kawaida
Dominika ya IV ya Pasaka ni Dominika ya mchungaji mwema, Dominika ya kuombea miito
katika Kanisa. Jambo la kwanza Mama Kanisa anatualika kusali kwa ajili ya miito na
pili kuijenga kuanzia ngazi ya familia hadi kanisa la ulimwengu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu
juu ya miito unatumbusha kwamba, miito ni alama ya matumaini yanayosimikwa katika
imani.
Baada ya kupokea ujumbe wa Papa tunasonga mbele tukiuunganisha na Neno
la Mungu likitufundisha nia ya Mungu ya kututaka sisi tukue katika kujitoa kwa mapendo
zaidi, mapendo ambayo yanadai mabadiliko ya ndani, kinyume na Wayahudi ambao kadiri
ya Neno la Mungu wanakwamisha mafundisho juu ya Neno la Mungu. Hata hivyo kwa kuwa
Bwana na Baba yake ni wamoja na nguvu yao yapita kila aina ya nguvu basi wapinzani
hawataweza kulishinda Neno la Mungu na mafundisho yake.
Katika somo la kwanza
Mtakatifu Paulo na Mtakatifu Barnaba wako katika safari ya kimisionari na wanatenda
kazi ya Bwana wakiongozwa na nguvu ya ufufuko. Katika ufanisi wa kazi hiyo wanakumbana
na vikwazo mbalimbali na mojawapo ni upinzani toka kwa Wayahudi. Wanafanyiwa fitina
na kukatishwa tamaa, lakini kwa kuwa wamejitoa kiaminifu na wakijitafiti wajibu wao
mbele ya Mungu wanakaza kamba na kusonga mbele.
Bwana yu pamoja nao, kama
kawaida kwani mtenda kazi ya Bwana hakosi msaada na nguvu ya Mungu. Nasi basi mpendwa
kazi ya uinjilishaji katika ulimwengu wa leo inao upinzani na hata wakati fulani upinzani
usi ona miguu wala mikono! Kumbe, wajibu wetu katika hali hii kwanza ni kukaa chini
na kutafakari kwa kina nini maana ya alama hiyo, na kisha kutoa jibu lililojaa upendo
wa kimungu ndani mwake. Jambo moja la kutuongoza ni kwamba sisi tu watu wake na kondoo
wa malisho yake na hivi lazima tumtegemee mchungaji wa kondoo.
Sehemu ya Injili
ya Mt Yohane inatufundisha juu ya upendo wa Mungu kwa wanadamu. Kawaida sura ya 10
ya Injili ya Yohane ni tafakari juu ya mchungaji mwema. Kwanza mchungaji mwema ni
Bwana wetu Yesu Kristo ambaye anazo sifa zote za mchungaji mwema, sifa ya kwanza ikiwa
ni kuwajua kondoo wake wote, yaani kujua shida zao, mahitaji yao na wema wao.
Jambo
jingine muhimu ni lile pia la kuwafundisha waziwazi anachotaka, alivyo yeye mwenyewe,
kumbe ni mwalimu ambaye anataka wanafunzi waweze kuwa na maarifa ya kumtambua mwalimu
wao. Hii ni alama ya upendo, ni alama ya kuondoa ubaguzi na mipaka katika muunganiko
wetu na Bwana. Bwana anasema nao wanijua mimi!.
Lengo la Bwana katika fundisho
hili ni kutaka kusema lazima watu wote wafikie uzima wa milele, kamwe hata mmoja asipotee.
Katika hili Bwana anasema watu ninaowajua mimi ni wale ambao amenipa Baba yangu, kumbe
yeye na Baba yake wako wamoja na lazima atimize mapenzi ya Baba yake.
Mpendwa,
unayenisikiliza, katika Somo la Pili tunapata kumwona Mtakatifu Yohane yuko katika
maono, anaona mkutano mkubwa ukizunguka kiti cha enzi na kila mwanamkutano amevaa
mavazi meupe na anayo majani ya mitende. Mara moja anauliza ni nani hawa na mzee anajibu
ni wale waliofua mavazi yao katika mwanakondoo, na sasa Mwanakondoo yuko katikati
yao.
Mpendwa, Mtakatifu Yohane anataka kutuonesha matunda ya kazi ya kimisionari
ambayo tutayapata hapo baadaye. Wale walio na mavazi meupe maana yake ni wale waliokubali
kuishi mapendo kamili, mapendo ya ndani wakiongozwa na Bwana ambaye daima yuko nasi
kwa njia ya Neno lake na kwa njia ya Sakramenti zake.
Ni wale ambao Bwana
aliwajua sauti za ona wao wakajua sauti yake na hivi wanafurahi naye katika kiti cha
enzi cha mbinguni. Wanafurahi na Mchungaji mwema ambaye hapotezi hata kondoo mmoja
cha msingi ujue sauti yake na kumfuata.
Mpendwa, hawa ndugu ambao wanamzunguka
mwanakondoo wanoneshwa katika alama ya mavazi meupe, ikiwa ni ishara ya furaha na
utu wema. Katika kipindi cha Pasaka mama kanisa amechagua mavazi meupe akiashiria
furaha tuipatayo kutoka ufufuko na ukiwa ni mwaliko wa furaha ya milele. Matawi ya
mitende ni alama ya ushindi baada ya kazi yao nzito hapa duniani. Nawe katika maisha
yako fanyeni yote vema na mbeleni kuna ushindi na vigelegele mbinguni.
Mpendwa,
ndiyo kusema njaa na kiu ya haki hapa duniani tuiishiyo haitakuwepo mbinguni, kumbe
mateso kama sehemu ya imani yetu yana mwisho tunapokutana na Bwana katika kiti chake
cha enzi.
Mpendwa mwana wa Mungu ninakualika daima kuiga mfano wa Mt. Paulo
kuvumilia magumu na matukano yatokanayo na imani, na ukisha vumilia yote sasa utaifuata
sauti ya Mchungaji mwema itujiayo kila siku kwa njia ya Kanisa na mwisho kuna zawadi
ya uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre
Richard Tiganya C.PP.S.