2013-04-19 07:27:38

Askofu mkuu Josephat L. Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha anasimulia historia ya wito wake wa Kipadre!


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika ujumbe wa Maadhimisho ya Siku ya 50 ya Kuombea Miito inayofanyika Jumapili ya nne ya Kipindi cha Pasaka, anasema kwamba, inawezekana hata leo hii bado watu wakaendelea kusikia na kuitikia wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ikiwa kama imani ni hai katika Jumuiya na Familia za Kikristo. RealAudioMP3

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican katika mahojiano maalum na Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania, anabainisha kwa ufupi historia ya maisha yake kama Padre; yale mambo yaliyomvutia tangu akiwa kijana kabisa wa umri wa miaka minane: alipenda kwa namna ya pekee kusikia Mapadre wakiimba ile Sala ya Baba Yetu kwa lugha ya Kilatini, Pater Noster! Akamwona mjomba wake amepewa Daraja Takatifu la Upadre, lakini akaendelea kubaki kuwa ni Mwafrika!

Askofu mkuu Lebulu anasema, msaada mkubwa katika maisha na wito wake wa Kipadre aliupata kutoka kwa Mama yake mzazi ambaye alibahatika kupata msingi thabiti wa maisha ya Kikristo kwani alifundishwa na Masista wa Damu Takatifu ya Yesu.

Alimwambia asiwe na wasi wasi wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani zake hata kama alikuwa ni mtoto wa kwanza wa kiume kwenye familia kwani "watoto ni maua ya Mungu, anaweza kuyachuma kwa ajili ya kupambia Altare yake na mengine akayaacha yaendelee kukua na kukomaa hata kuzaa maua mengine.

Askofu Lebulu alizaliwa tarehe 13 Juni 1942, Kisangara, Jimbo Katoliki la Same. Kunako mwaka 1958 alijiunga na Seminari Ndogo. Mwaka 1963 hadi Mwaka 1968 alipata majiundo yake ya Kipadre Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi na Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora. Akiwa Seminari kuu hamu ya kutaka kuhubiri ikashika kasi ya ajabu na kishawishi cha kusoma zaidi hadi kieleweke kikazidi kupamba moto. Tarehe 11 Desemba 1968 akapewa Daraja Takatifu la Upadre.

Tarehe 12 Februari 1979 akateuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Same. Tarehe 24 Mei 1979 akawekwa wakfu kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Same. Tarehe 28 Novemba 1998 akateuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha na kuwekwa wakfu hapo tarehe 16 Machi 1999.

Mambo baaado kabisa, usikose kujiunga nasi tena ili kusikiliza sehemu ya pili na ya mwisho ya historia ya Askofu mkuu Josephat Lebulu, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 Tangu Siku ya Kimataifa ya kuombea Miito ilipozinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Paulo wa Sita.







All the contents on this site are copyrighted ©.