2013-04-18 08:13:52

Kanisa ni mali ya Kristo!


Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anabainisha kwamba, Kanisa ambalo lilianzishwa na Kristo yapata miaka elfu mbili iliyopita ni mali ya Kristo mwenyewe anayeendelea kuliongoza kwa njia ya Roho Mtakatifu. RealAudioMP3

Licha ya kinzani, magumu na changamoto mbali mbali zinazoendelea kutolewa dhidi ya Kanisa, lakini bado Kanisa litaendelea kustawi na kushamiri na kamwe haliwezi kutishwa na kuogofya na malimwengu pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari za Kanisa nchini Nigeria, CNSN, Askofu mkuu Kaigama ameyabainisha hayo wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 150 tangu Shirika la Utume Barani Afrika, (SMA) lilipotua nanga kwa mara ya kwanza nchini Nigeria. Sherehe hizi zilikuwa pia ni sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Askofu mkuu Kaigama anasema, inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya vyombo vya upashanaji habari ambavyo vimejikita kutangaza mapungufu ya Kanisa kutokana na udhaifu wa Watoto wake na kusahau mchango mkubwa ambao Kanisa linaendelea kutoa katika ustawi na maendeleo endelevu kwa watu wengi duniani. Huu ni mchango wa Mapadre na Watawa wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa kutoa huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo.

Kanisa linakubali kukosolewa kama njia ya kufanya toba na wongofu wa ndani kutokana na mapungufu ya kibinadamu yanayooneshwa na watoto wake. Lakini, haya yote ni matokeo ya kuporomoka kwa misingi ya bora ya maisha ya kifamilia na madhara yake ndiyo hayo yanayojionesha pia kwa Jamii nyingi kukengeuka katika misingi ya maadili na utu wema. Maisha ya useja yanapaswa kuchukuliwa kuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Ni changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na Jirani, kila Padre akijitahidi kuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Katika safari ya maisha ya kiroho kama hii, kuna baadhi ya Mapadre huanguka na kuelemewa na ubinadamu wao, lakini ikumbukwe kwamba, bado kuna idadi kubwa ya Mapadre ambao ni waaminifu katika maisha yao ya useja, jambo ambalo kamwe haliwezi kubezwa.

Askofu mkuu Kaigama amelipongeza Shirika la Utume Barani Afrika kwa kujitosa kimasomaso bila woga wala makunyanzi kwenda nchini Nigeria kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Matunda ya kazi na utume huu yanaonekana wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa kwa mara ya kwanza na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili.

Ni mwaliko na changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaendelea kutumia vyema baraka na neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Mashirika ya Kitawa na Kimissionari yawekeze zaidi na zaidi katika majiundo ya Mapadre na Watawa wazalendo ili yaendelee kutoa huduma za kichungaji katika nchi za Kimissionari badala ya kukata tamaa na kufunga vilago ili kurudi Ulaya.








All the contents on this site are copyrighted ©.