Kanisa halina budi kuwa na sera na mikakati inayolenga kuimarisha shughuli za kimissionari
kwa ajili ya Uinjilishaji
Baba Mtakatifu Francisko ameandika ujumbe kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina
wanaoendelea na mkutano wao wa mwaka, unaotarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 20 Aprili
2013 kwa kuwataka kuweka sera na mikakati ya kichungaji yenye mwelekeo wa kimissionari,
daima wakifanya rejea kwenye hati za Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika
ya Kusini uliofanyika mjini Aparecida, "kutweka hadi kilindini".
Baba Mtakatifu
anaomba msamaha kwa kutoweza kuhudhuria kwenye mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Argentina kutokana na majukumu aliyokabidhiwa hivi karibuni na Mama Kanisa. Kwa namna
ya pekee, anawataka Maaskofu kuonesha ujasiri wa kutoka ndani na kuwaendelea wale
waliotawanyika sehemu mbali mbali za Argentina, watu wenye kiu na hamu ya kutaka kukutana
na Yesu kristo Mkombozi wa Ulimwengu.
Kanisa linalojiangalia lenyewe limepitwa
na wakati, changamoto kwa viongozi wa Kanisa wakishirikiana na waamini kutweka hadi
kilindini ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu
wa utandawazi uliosheheni ukanimungu pamoja na mmong'onyoko wa maadili na utu wema.
Ni wakati kwa Mama Kanisa kujifunga kibwebwe na kujitosa ulimwenguni ili kuwainjilisha
walimwengu, waone na kuonja utamu wa Injili.
Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe
wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kwa kuwaomba waendelee kumwombea katika
maisha na utume wake; ajifunze zaidi na zaidi kusikiliza kile ambacho Mwenyezi Mungu
anataka kwa ajili ya Kanisa lake na wala si kwa ajili ya kutekeleza matakwa yake binafsi.
Wakati
huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina katika mkutano wake wa Mwaka linabainisha
kwamba, ili kuweza kuleta mageuzi ya kweli katika mfumo wa haki, kuna haja ya kufanya
tafakari ya kina, itakayowashirikisha wadau mbali mbali, ili kila mtu kwa nafasi na
dhamana yake aweze kuchangia mawazo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
nchini Argentina. Mambo haya hayana budi kugusa: Haki, Demokrasia na Katiba ya Nchi
ambayo kimsingi ni sheria Mama.
Rais Cristina Fernandez Kirchner wa Argentina
amekwisha toa maelekezo ya muswada wa sheria unaopaswa kufanyiwa mabadiliko makubwa
nchini humo ili watu kwa njia ya kidemokrasia waweze kuonana na wadau wa sheria, mawaziri
na watumishi wengine wa Serikali: Ukweli na uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya
mahakama; uwezekanao wa wananchi kupima ufanisi wa mihimili mikuu ya nchi yaani: Bunge,
Mahakama na Serikali.
Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linasema kwamba,
haya mambo yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa vinginevyo demokrasia inaweza kugeuzwa
kuwa ni uwanja wa fujo na vurugu za kijamii.