Huduma kwa maskini na wanyonge itolewe kwa moyo wa ukarimu na unyenyekevu!
Padre Germini Longio Lukoka kutoka Jimbo Katoliki la Same, Tanzania ni kati ya waamini,
mahujaji na watalii waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican, Jumatano tarehe 17 Aprili 2013 wakati wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko.
Padre Lukoka
katika mahojiano na Radio Vatican anasema, kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika
utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anaendelea kutoa changamoto kubwa kwa Waamini
kuhudumia katika hali ya unyenyekevu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kama alivyofanya Kristo mwenyewe katika Fumbo
la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo
na ufufuko wa Kristo.
Anasema, tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza
Kanisa Katoliki, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro umekuwa ukifurika kwa umati
mkubwa wa waamini, mahujaji na watalii. Ameonesha upendo wa pekee kwa wanyonge, akina
mama na watoto.
Hii ni changamoto kwanza kabisa ya kuwalinda na kuwathamini
watoto kwa kuwapatia malezi bora: kiroho na kimwili ili waweze kukua na kukomaa katika
hekima na kimo. Wanawake wawezeshwe kikamilifu ili waweze kutekeleza utume na dhamana
yao katika maisha ya Kijamii na Kikanisa.
Padre Longio anahitimisha mahojiano
haya na Radio Vatican akimtakia kheri na fanaka Baba Mtakatifu Francisko anapojiandaa
pia kusherehekea Siku ya Mtakatifu Joji, Shahidi, somo wake hapo tarehe 23 Aprili
2013.