2013-04-17 08:41:26

Imani kwa Kanisa na umuhimu wake katika maisha ya kijamii


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea kukuletea ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Leo tunaangalia kuhusu: Imani kwa Kanisa na umuhimu wa kuipyaisha imani hiyo. RealAudioMP3
Imani kwa Mungu na kwa Neno lake
1. “Nasadiki kwa Mungu mmoja”. Msingi wa imani yetu ni Mungu katika Nafsi Tatu; yaani, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mungu anayetupatia zawadi ya imani anatutaka tumtolee shukrani kwa kuiishi zawadi hii tukiwa tumeunganika naye katika Utatu wake Mtakatifu. Katika Injili ya Yohane, Yesu alipowaasa wafuasi wake wasikitendee kazi chakula kiharibikacho (Rej. Yn 6: 27) wao waliuliza wakitaka kujua wafanye nini basi: “Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?” (Yn 6:28). Hili ni swali ambalo tunaweza kulifanya kuwa letu katika kipindi hiki cha Mwaka wa Imani, na bila shaka, katika maisha yetu yote. Yesu anawajibu akisema: “Hii ndiyo kazi ya Mungu: mmwamini yeye aliyetumwa na yeye” (Yn 6:29). Humo ndimo ulimo utimilifu wote wa mpango wa Mungu anayejidhihirisha katika Utatu Mtakatifu. “Kukiri imani katika Utatu Mtakatifu – Baba, Mwana na Roho Mtakatifu – ni kuamini katika Mungu mmoja ambaye ni Upendo (rej. 1 Yn 4:8): Baba, ambaye katika utimilifu wa wakati alimtuma Mwanae kwa ajili ya wokovu wetu; Yesu Kristo, ambaye kwa fumbo la kifo chake na ufufuko aliukomboa ulimwengu; Roho Mtakatifu, ambaye analiongoza Kanisa katika karne zote tunaposubiri ujio mtukufu wa Bwana.”

2. Imani kwa Mungu inakuwa ni tendo linalotuinua kupitia tendo la “utii wa imani”: “Utii wa imani lazima apewe Mungu anayejifunua (Rum 16:26; taz. Rum 1:5; 2Kor 10:5-6). Kwa imani mwanadamu hujikabidhi kikamilifu na kwa uhuru mikononi mwa Mungu, akitoa kwa Mungu mwenye kufunua “heshima kuu ya akili na utashi”, na akikubali kwa hiari ufunuo anaopewa na Yeye. Ili imani hii iweze kutekelezwa, mtu hana budi kutanguliwa na kusaidiwa na neema ya Mungu. Kadhalika hana budi kuwa na msaada wa ndani wa Roho Mtakatifu anayesukuma moyo na kumwelekeza kwa Mungu, na anayefunua macho ya akili na anayewapa “watu wote utamu katika kuukubali na kuuamini ukweli”. Roho Mtakatifu huyohuyo hukamilisha imani daima, kwa njia ya mapaji yake ili ufunuo ueleweke kwa undani zaidi.”

3. Neno la Mungu linabaki kuwa ni msaada usiopimika unaotusaidia kung’amua kujifunua huku kwa Mungu. Imani yetu katika Kristo hulishwa kwa neno la Kristo mwenyewe. “Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Rum 10:17). Neno la Mungu linailisha imani yetu na kutupatia hakikisho la kile tusichokiona na kukigusa sasa kupitia milango yetu mitano ya fahamu. Imani inakuwa ni mlango wa sita wa fahamu ulio na umuhimu wa juu kwani inatusaidia kutamani yale ambayo jicho halijapata kuona wala sikio kusikia (Rej. 1Kor 2:9). “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu” (Rum 10:10).

Imani kwa Kanisa
4. “Nasadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume”. Kanisa linabaki kuwa “Mama na Mwalimu” wa imani na ni chombo cha kimungu kinachowaunganisha watu na Mungu na baina yao. Kwa sababu hiyo Mt. Ireneo wa Lione anatukumbusha kuwa, “Lilipo Kanisa, yupo Roho wa Mungu: alipo Roho wa Mungu lipo Kanisa na neema zote.” Kwa maneno mengine ndio kusema, lilipo Kanisa la kweli lililoanzishwa na Kristo juu ya msingi wa Mitume hapo imani ya kweli ipo, kwa sababu, “Kanisa la Mungu aliye hai”, ni “nguzo na msingi wa kweli” (1Tim 3:15). Hata hivyo, ilipo imani hazikosekani changamoto. Kwa sababu, “hatusadiki tu kwa Kanisa, bali wakati huo huo sisi nasi ni Kanisa.” Tunatambua wazi kwamba huku kuwa Kanisa ni safari ya wongofu. Ni safari ya wongofu kwa kuwa ndani ya Kanisa wadhambi na watakatifu wanapata nafasi, lakini wote wakialikwa kukua katika njia ya wongofu. “Kanisa … ambalo huwakumbatia wakosefu ndani yake, na wakati uleule ni takatifu na linahitaji kutakaswa, haliachi kamwe kutubu na kujitengeneza upya.”
5. Safari yetu ya kukua katika imani ndani ya Kanisa inaifanya nafasi ya Kanisa kwa wokovu kuwa ni ya muhimu sana. Umuhimu wake unatokana na ukweli kwamba lenyewe ni Mwili wa Fumbo (Kol 1:18) wa Kichwa ambaye ni Kristo mwenyewe. Ndiyo maana, Kanisa “ni mwezi wa kweli. Kutoka katika mwanga usiokuchwa wa nyota ya kidugu, linapata mwanga wa umilele na wa neema. Kimsingi, Kanisa haliangazi mwanga ulio wake kwa asili, bali mwanga wa Kristo. Kanisa linapata mng’ao wake kutoka kwenye jua la haki, ili baadaye liweze kusema: mimi ninaishi, lakini si mimi bali Kristo anaishi ndani yangu (Gal 2:).” Ni kutokana na uhusiano huu uliopo kati ya Kristo na Kanisa ndio maana Mt. Sipriano hasiti kutusaidia kutambua kuwa; “Kama hatuna Kanisa kama mama, hatuwezi kuwa na Mungu kama Baba.”
Imani iliyo hai
6. Imani ambayo mwanzo wake ni Mungu mwenyewe, inapaswa kuwa hai na kwa hulka yake, kila kilicho na uhai kinakua. Mitume walipoyasikia mafundisho ya Yesu aliyeonya juu ya watu kuwa chanzo cha makwazo, Mitume wanaomba kuongezewa imani: “Bwana, tuongezee imani” (Lk 17:5). Mahali pengine tunakutana ya Yesu anayemponya yule kijana mwenye pepo. Pamoja na imani ya baba wa kijana huyu, bado alimwambia Yesu, “ukiweza neno lolote, utuhurumie” (Mk 9:22). Yesu anamjibu akisema: “Yote yawezekana kwake aaminiye” (Mk 9:23). Baba wa kijana anamalizia kwa kusema: “Naamini, nisaidie kutoamini kwangu” (Mk 9:24). Haya yalikuwa baadhi ya matukio katika Injili ambayo yanatufunulia ukweli kwamba, imani kwa asili yake inakua na inakua vema kama inakuzwa kwa msaada wa neema ya Kristo.
7. Inapotokea kwamba kuna kutetereka katika makuzi ya imani ni wajibu wetu kukumbushana na kuhimizana, ili tuweze kuamka na kusimama tena katika imani. Huu ni mwaliko wa kurudi tena kwenye misingi ya imani na kujipima ili kuona kama maisha yetu bado yamesimama katika msingi wa imani au tumeanza kupotoka. Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho anawapa changamoto akisema: “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekua katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu?” (2Kor 13:5). Mtume Paulo anawataka wajipime kuona ni kwa kiasi gani na ni kwa namna gani waamini wa Korintho wamekua katika imani. Wakati kwa upande mmoja imani hujaribiwa na Mungu, kwa upande mwingine Mtume Paulo anatushauri tujipe nafasi za kujijaribu wenyewe ili tuone kama tunakua au tunadumaa katika imani. Zipo namna nyingi za kujijaribu wenyewe katika imani, lakini njia ya uhakika kabisa ya kujipima ni kuangalia ni kwa namna gani tunakua katika fadhila zile mbili zingine za kimungu; yaani matumaini na mapendo.








All the contents on this site are copyrighted ©.