Baba Mtakatifu Francisko ametuma salama za rambi rambi kwa Kardinali Seàm O' Malley,
Askofu mkuu wa jimbo kuu la Boston, Marekani kutokana na mauaji ya kinyama yaliyotokea
Jumatatu tarehe 15 Aprili 2013 wakati wa mashindano ya mbio za Marathon na kusababisha
watu watatu kupoteza maisha na wengine 141 kulazwa hospitalini.
Ujumbe wa
Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu
wa Vatican. Anasema, anaungana na wote wanaomboleza kutokana na kuondokewa na ndugu,
jamaa na marafiki zao. Anawakumbuka pia wote waliopatwa na majeraha ili waweze kupona
haraka na kuendelea na shughuli zao. Anawaomba wasamaria wema kuendelea kutoa msaada
wa hali na mali kwa waathirika wa tukio hili.
Kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu
anawaomba wananchi wa Marekani kushinda uovu kwa wema; daima wakijitahidi kujenga
na kuimarisha haki, uhuru na usalama hata kwa kizazi kijacho.