2013-04-16 10:06:39

Ujumbe kutoka Yerusalem una matumaini ya kumwona Papa Francisko akitembelea Mashariki ya Kati


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 15 Aprili alikutana na kuzungumza na Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu pamoja na ujumbe wake. Kwa pamoja wamezungumzia kuhusu machafuko ya kisiasa huko Mashariki ya Kati na kwa namna ya pekee hali ya vita nchini Syria pamoja na idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi ambao kwa sasa wanahitaji msaada wa dharura.

Kanisa kwa upande wake, linaendelea kuonesha mshikamano wa dhati na watu hawa ili kamwe wasijisikie pweke. Ni matumaini ya Patriaki Twal kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ataweza kufanya hija ya kichungaji huko Mashariki ya Kati, ili kuweza kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Patriaki Twal anasema, Baba Mtakatifu amewasikiliza kwa umakini mkubwa akitaka kufahamu hali halisi, ili kuchangia katika mchakato wa kutafuta na hatimaye, kudumisha amani.

Mara baada ya mkutano na ujumbe wa Patriaki Twal, Baba Mtakatifu Francisko alijiunga pamoja nao kwa chakula cha mchana, jambo ambalo limewaacha wajumbe wengi wakiwa wameshikwa na butwaa kwa kutoamini unyenyekevu, upendo na mshikamano wa kidugu uliooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu Msaidizi William Shomali wa Upatriaki wa Yerusalemu anasema, anaporudi Jimboni mwake, atawasimulia waamini upendo mkubwa unaooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Kanisa; anayesali na kuwaombea waamini walioko kwenye Nchi Takatifu, mahali ambako Yesu aliishi, akateswa, akafa na hatimaye, kufufuka kutoka katika wafu.







All the contents on this site are copyrighted ©.