2013-04-16 07:48:55

Mapapa wanatofautiana kwa karama na vipaji, lakini lengo ni kujenga na kuliimarisha Kanisa la Kristo


Kardinali Zenon Grocholewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, katika mahojiano maalum na Shirika la Habari za Kanisa, Zenit mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kama mwanzo wa utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anasema kwamba, kwa hakika Kanisa limempata kiongozi anayefahamu kusoma alama za nyakati, atakayelisaidia Kanisa kugusa tena akili na mioyo ya watu kutokana na unyenyekevu wake. RealAudioMP3
Baba Mtakatifu Francisko, Myesuit wa kwanza kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu na Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini, anaendelea kutoa changamoto nyingi kwa Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Kuchaguliwa kwake ni zawadi ya Roho Mtakatifu na kielelezo kwamba, Kanisa ni la Kristo mwenyewe na haijalishi mtu anatoka katika nchi gani.
Uwepo wake utasaidia kuendeleza mchakato wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Hii ni zawadi kubwa kwa Kanisa la Kiulimwengu, lakini wananchi wa Argentina wanayo haki ya kufurahi na kumshukuru Mungu kwa kupata kiongozi ambaye anafahamu mateso na mahangaiko yao!
Kardinali Zenon Grocholewski anasema kwamba, Makrdinali walikuwa ni vyombo ambavyo vilitumiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu kufanya uchaguzi na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akachaguliwa kumrithi Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliyeng’atuka kutoka madarakani kwa utashi na uhuru kamili, ili kutoa fursa kwa Kiongozi mwingine kuweza kuongoza kwa ari, kasi na nguvu mpya Kanisa ambalo daima ni mali ya Kristo anayelikirimia watu wa kuliongoza kadiri ya mapenzi yake.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili ni kiongozi ambaye alifungua malango ya Kanisa kwa watu katika nchi mbali mbali, anakumbukwa sana kwa kufanya hija za kichungaji zilizosaidia kuamsha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa Familia ya Kimataifa. Alilichangamotisha Kanisa kuwa na ujasiri na ari ya kujitosa bila woga katika dhamana ya Uinjilishaji unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alikuwa ni Baba, Mwalimu na Katekista mkuu ambaye alitumia akili, maarifa, ujuzi na mang’amuzi yake kwa ajili ya kuunganisha imani na akili ya mwanadamu katika kutafuta na kukumbatia ukweli ambao ni Mungu mwenyewe. Ni kiongozi aliyekazia kwa namna ya pekee majadiliano kitamaduni na kisayani, daima Mungu na mwanadamu wakipewa kipaumbele cha kwanza.
Kanisa sasa linaendelea kupeta kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye ni mtu mwenye maneno machache, lakini matendo yake yanaacha alama ya kudumu katika maisha na mioyo ya watu, kama inavyojionesha hadi sasa.

Ni kiongozi mwenye sanaa na uwezo wa kuzungumza na kugusa mioyo ya watu. Viongozi wote hawa wanaonesha karama na mapaji mbali mbali ya Roho Mtakatifu katika kutembea katika mwanga wa Kristo mfufuka, ili kushiriki katika ujenzi wa Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.
Katika hotuba zake ambazo ametoa kwa watu mbali mbali tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa, amesisitizia kwamba, Kristo ndiye nguvu na jeuri ya Kanisa. Ni changamoto kwa kila mwamini kujikita katika sala, upendo na mshikamano wa kidugu, kwa ajili ya mafao ya wengi na utunzaji bora wa mazingira.








All the contents on this site are copyrighted ©.