2013-04-16 09:03:34

Jumuiya ya Kimataifa inaalikwa kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia nchini Syria


Viongozi mbali mbali wa kidini nchini Uingereza wameendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Syria kwani mateso ya wananchi wa Syria kwa sasa yamevuka kiwango cha uvumilivu wa kibinadamu.

Tangu mwaka 2011, zaidi ya Wakristo 1,000 wameuwawa kikatili; Makanisa, shule na zahanati zipatazo 40 zimeharibiwa kutokana na machafuko ya kidini yanayoendelea nchini Syria. Hakuna amani wala usalama kiasi kwamba, Ukanda wa Mashariki ya Kati uko hatarini kwa sasa. Kwa miaka mingi Syria ilikuwa inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Lebanon, Iraq na katika nchi nyingine jirani, lakini sasa hakuna tena amani wala usalama.

Haya yamo kwenye ujumbe wa Patriaki Gregorios wa tatu kutoka Syria anayewaalika viongozi mbali mbali wa kidini kuombea amani na kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kutoa kipaumbele cha pekee, ili kuokoa maisha ya watu wengi kutokana na vita inayoendelea nchini Syria.

Wananchi wa Syria wanapaswa kuchukua maamuzi magumu yaani kuendelea kubaki nchini mwao ili kukabiliana na kifo uso kwa uso au kukimbia ili kusalimisha maisha yao!







All the contents on this site are copyrighted ©.