Juhudi za Makanisa Zimbabwe katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki na amani
kuelekea kwenye uchaguzi mkuu
Wananchi wa Zimbabwe wameanza maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
mwaka huu, baada ya kupitisha Katiba kwa kura ya maoni na hivyo kufanya mabadiliko
makubwa yanayopania pamoja na mambo mengine, kupunguza madaraka makubwa aliyokuwa
nayo Rais, kusimamia haki msingi za binadamu pamoja na kudumisha misingi ya haki na
amani.
Kwa kuzingatia
historia ya Zimbabwe kwa miaka ya hivi karibuni, iliyopelekea machafuko ya kisiasa
na hatimaye kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Baraza la Makanisa Zimbabwe
limeunda Tume ya Kiekumene ya Wasimamizi wa Uchaguzi mkuu, yenye dhamana ya kukoleza
moyo wa majadiliano, ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho
wa kitaifa.
Tume hii inatekeleza wajibu wake kabla, wakati na baada ya uchaguzi
mkuu na inasimamiwa na Tenda Maregere. Haya ni malengo ambayo Baraza la Makanisa Zimbabwe
lilijiwekea kwa kitambo kidogo, kwa sasa yanafanyiwa utekelezaji wake, kadiri ya taarifa
iliyotolewa na Shirika la Habari la Misna.
Makanisa nchini Zimbabwe yamekuwa
yakichangia kwa kiasi kikubwa katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani,
upendo na umoja wa kitaifa, bila kusahau upatanisho pale ambapo kinzani na migogoro
ya kisiasa ilipojitokeza; mambo ambayo yamekuwa ni sehemu ya historia ya wananchi
wa Zimbabwe tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru kutoka katika utawala wa Mwingereza.
Tume
ya Mabaraza ya Makanisa pamoja na mambo mengine inapania kukuza moyo wa majadiliano
miongoni mwa wananchi wa Zimbabwe, kudhibiti mchakato mzima wa upigaji kura ili haki,
uhuru na ukweli viweze kutawala na hatimaye, Zimbabwe iweze kuwapata viongozi watakaochaguliwa
kwa kura halali wakitambua dhamana na wajibu wao katika kuiendeleza nchi yao. Tume
itakuwa na wajibu wa kusema haraka iwezekanavyo pale ambapo kutakuwepo na ukiukwaji
wa haki msingi za binadamu.
Vyama vikuu vya upinzani vinavyotoana jasho kwa
sasa ni ZANU-PF kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe pamoja na Chama cha Democratic
Movement for Change kinachoongozwa na Waziri mkuu wa Zimbabwe Bwana Morgan Tsvangirai;
wapinzani wakuu waliopelekea machafuko ya kisiasa nchini Zimbabwe kunako mwaka 2008.